MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amewekwa mahabusu na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa madai ya kukiuka utaratibu wa Mahakama.


Mbowe alijisalimisha mwenyewe katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam saa 11 jioni jana, akiambatana na mwanasheria wake Mabere Marando.


Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Marando alidai walipofika katika kituo hicho cha Polisi, Mbowe aliwekwa mahabusu na polisi walisema wanafanya mipango ya kumpeleka Arusha kujibu mashitaka yanayomkabili ya kuidharau Mahakama na kushindwa kuhudhuria kesi.


Mwanasheria huyo alidai awali polisi walisema kwamba mara baada ya kujisalimisha, Mbowe ambaye Marando alisema ana kinga za kisheria za kuzuia kukamatwa na polisi akiwa kama Mbunge, angepelekwa Arusha bila kuwekwa mahabusu lakini alipofika kituoni hapo alitiwa

ndani.

“Sasa hivi (saa 12 jioni jana) wanasema tuwaachie wenyewe watajua ni utaratibu upi watautumia kumsafirisha Mheshimiwa Mbowe kwenda Arusha, kwa hiyo hatujui ni saa ngapi watampeleka Arusha.


“Lakini sisi kesho asubuhi tutamletea ugali, tukimkuta tutampa ale, tusipomkuta tutajua

tayari amepelekwa Arusha,” alisema Marando.

Alisema hata hivyo kwa mujibu wa polisi, Mbowe anatakiwa apandishwe kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Arusha, kesho.


“Hii ndio Serikali ambayo haijali wala haizingatii utawala wa sheria, nadhani Spika wa Bunge, Anne Makinda anapaswa kulitolea tamko suala hili,” alidai Marando.


Mwanasheria huyo alidai pamoja na Serikali kukiuka sheria na kuchukua hatua hiyo ili kumkomesha kiongozi huyo wa Chadema hatua hiyo haikatishi tamaa chama hicho bali ni chachu ya kuiondoa madarakani CCM.


“Wala hatuwezi kuwashitaki bali tutakachokifanya ni kuwaeleza wananchi nini Serikali ya CCM inakifanya ili kuua nguvu za viongozi wa upinzani, na tutawaambia dawa pekee ni kuiondoa CCM madarakani,” alisema Marando.


Juzi Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alisema Mbowe hakuhudhuria mahakamani kwa kuwa amekuwa akihudhuria vikao vyote vya kamati mbalimbali za Bunge.


Lissu, ambaye pia ni mwanasheria, alisema mila na desturi za kibunge za Jumuiya ya Madola zinataka kinga ya wabunge dhidi ya kukamatwa iwe na nguvu wakati wa mkutano wa Bunge pamoja na muda muafaka wa kutosha kabla na baada ya mkutano wa Bunge.


“Hivyo Mbowe akiwa ndani ya gari lake la ofisi, haruhusiwi kukamatwa, akiwa nyumbani kwake, akiwa humu ndani na hata akiwa barabarani ni eneo la Bunge kwani yuko hapa kuhudhuria vikao vya Bunge,” alisema Lissu.


Lakini wakati Lissu akitetea uamuzi wa Mbowe kutokwenda mahakamani, hakufafanua kwa nini wabunge wengine wa Chadema waliokuwa katika kesi hiyo, walitii na kufika mahakamani kama walivyotakiwa.


Wabunge hao ni pamoja na Godbless Lema wa Arusha Mjini na Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini alituma mdhamini, jambo lililotafsiriwa kuwa waliheshimu Mahakama.


Pia juzi hiyo, wakati Mbowe akidai alikuwa sahihi kutokwenda mahakamani kwa madai kuwa ana shughuli nyingi za kuandaa bajeti mbadala, huku akiungwa mkono na Lissu, mkoani

Arusha mdhamini wake, Julius Magwe alijisalimisha mahakamani.

Magwe alijisalimisha katika mahakama hiyo saa 5.15 huku akiambatana na wafuasi mbalimbali wa chama hicho na wakili wa upande wa utetezi, Method Kimomogoro.


Wakili Kimomogoro alidai kuwa mdhamini huyo alikuwa akihudhuria mahakamani siku zote lakini isipokuwa siku hiyo ambayo ulitolewa uamuzi wa kukamatwa yeye na Mbowe kwa

kuwa alikuwa ugonjwa.

Ili kuongeza nguvu katika utetezi wake, Magwe aliwasilisha vielelezo mahakamani hapo ikiwemo cheti cha daktari aliyemruhusu kupumzika.


Wakati huo huo, Mwandishi Wetu kutoka Arusha aliripoti kwamba kumekuwa na ujumbe wa simu uliokuwa ukisambazwa kuhamasisha wananchi kwenda kumlaki Mbowe mahakamani kesho.


Ujumbe huo umewataka wanachama na wafuasi wa Chadema kufikia mahakamani kumuunga mkono Mwenyekiti wao.