WASHITAKIWA watatu kati ya watano waliokamatwa miaka mitatu iliyopita wakituhumiwa kumuua mtoto mlemavu wa ngozi (albino), Ester Charles Juni 3 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora.
Jaji Laurence Kaduri aliyekuwa akisikiliza shauri hilo, aliwahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa hao, Charles Kalamuyi (zungu), Masumbuko Madada (Sumbu) na Merdadi Maziku (Machunda) kutokana na kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila shaka yoyote.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa takribani saa nne, mshitakiwa mwingine Peter Mahina, aliachiwa huru baada ya kukosekana ushahidi wa kumuunganisha wakati mshitakiwa wa tano Malalija Jiduta, alifariki dunia akiwa rumande wakati kesi hiyo haijaanza kusikilizwa.
Awali upande wa mashitaka ukiongozwa na jopo la mawakili watatu Neema Ringo, Prudence Rweyongeza na Janeth Sekule, uliiambia Mahakama kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Oktoba 19, 2008.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo katika kijiji cha Shilela Usala, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, washitakiwa walimuua mtoto huyo kwa kumkata mapanga sehemu za mabega.
Kwa mujibu wa madai hayo, baada ya kutenda unyama huo washitakiwa walikinga damu yake na kutokomea nayo na kumwacha mlemavu huyo akiwa hajitambui na baadaye akapoteza maisha kutokana na kuvuja damu nyingi.
Serikali katika kesi hiyo iliwasilisha mashahidi watano na kupitia mawakili wake iliomba Mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa kutokana na kitendo kibaya na cha kinyama walichofanya.
Washitakiwa kwa upande wao waliokuwa wakitetewa na mawakili Kamaliza Kayaga, Merdai Mutongole na Vedastus Lauriani waliiomba Mahakama iwaachilie huru wateja wao kwa madai kwamba hawakuhusika katika mauaji ya mtoto huyo, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na Jaji Kaduri.
0 Comments