Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,(Pichani juu) amesema uzinduzi wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utafanyika ifikapo Aprili 26, 2014 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar baada ya kukamilika.
Alisema hayo alipofungua semina elekezi kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu mchakato wa kuelekea kuundwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika katika Kituo cha Mtakatifu Gasper, mjini hapa jana.
“Ni matarajio ya serikali kuwa Katiba mpya itakuwa imekamilika na kuzinduliwa ifikapo tarehe 26 Aprili 2014, katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema Pinda.
Alisema Muswada wa Sheria kuhusu Mapitio ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 2011, utawasilishwa bungeni mwishoni mwa Mkutano wa Nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa mjini hapa, au mwanzoni mwa Mkutano wa Tano wa Bunge, utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Waziri Mkuu alisema Muswada huo utakapopitishwa na Bunge, taifa litakuwa limeanza rasmi mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuwa mstari wa mbele kuongoza mchakato huo kwa kuwahamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika zoezi la kutoa maoni yao kwa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuelekea kutungwa Katiba mpya, kuhusu Katiba wanayoitaka.
Pia aliwataka viongozi kutumia wasaa wa semina hiyo ili waweze kuwa walimu na wahamasishaji wazuri wa wananchi katika ushiriki wa kuundwa kwa Katiba mpya ya Nchi.
Alisema maeneo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika zoezi zima la Tume hiyo, ni nafasi na majukumu ya mihimili mitatu ya dola, ikiwamo Mahakama, Serikali na Bunge; pia masuala ya haki za binadamu na utawala bora.
Pinda alisema katika hatua ya kukusanya maoni ya wananchi, Tume itazunguka nchi nzima na kufanya mikutano ya hadhara ya ndani na kuwataka viongozi hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tume ili kuwezesha mikutano hiyo kufanyika kama ilivyokusudiwa.
Alisema ushirikiano huo ni kuhamasisha wananchi kuhudhuria katika mikutano hiyo na kuwezesha upatikanaji wa masuala yote muhimu katika uendeshaji wa mikutano.
Hata hivyo, aliwataka viongozi hao kuwaelimisha wananchi kuwa hatua iliyopo hivi sasa, siyo ya kutunga Katiba mpya, bali ni kuunda Tume hiyo.
Pia wawaelimishe viongozi kutoingiza siasa na kujiepusha kuwashawishi wananchi katika kutoa maoni yao, bali waache watoe maoni kwa uhuru au pasipo shinikizo lolote.
Vilevile, viongozi wajiepushe kuwa na upendeleo au ubaguzi wowote katika misingi ya kiimani, kijinsia na kiitikadi katika kutoa na kukusanya maoni yao.
Semina hiyo inalenga kuwawezesha viongozi hao kufahamu kwa undani maudhui ya Muswada huo, ambao umeainisha hatua mbalimbali zitakazopitia kuelekea mabadiliko ya Katiba ya Nchi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua semina hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, alisema ofisi yake imeona umuhimu kuandaa semina hiyo, baada ya kubaini kuwa katika hatua za mwanzo za mchakato wa kutunga Katiba mpya, baadhi ya wananchi hawana uelewa sahihi juu ya dhamira ya serikali kuhusu suala hilo.