Chama cha Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), kimetoa tamko kikitaka wanafunzi wote waliofukuzwa baada ya uongozi wa chuo hicho (Udom) kufunga vyuo vyao, warudishwe mapema ili kumaliza sehemu ya muhula wa masomo yao uliobaki.
Vyuo vya Udom vilivyofungwa na uongozi wa chuo hicho wiki chache zilizopita na hivyo kuwalazimu wanafunzi hao kurudi majumbani, ni Chuo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii (CHSS) na Chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Cive).
Hatua hiyo ilifikiwa na uongozi wa Udom, baada ya wanafunzi hao kugoma kuingia madarasani, wakidai kutekelezewa mahitaji maalum ya kozi zao, ikiwamo kompyuta aina ya laptop, kifaa cha kuhifadhia kumbukumbu (flash disk), kifaa cha kuwezesha mawasiliano ya kompyuta (modem) pamoja na mazoezi kwa vitendo (PT) kwa baadhi ya programu.
Tamko hilo, ambalo ni sehemu ya msimamo wa Udomasa kuhusu urudishwaji wa wanafunzi hao, lilitolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Paul Loisulie, mjini hapa juzi.
Alisema vyuo husika pamoja na uongozi wa Udom, wanapaswa kufanya utaratibu mapema iwezekanavyo ili wanafunzi hao waweze kurudi vyuoni kumaliza sehemu ya muhula wa masomo uliobaki. Mwenyekiti huyo alisema kama kuna hatua zozote za kinidhamu zitakazochukuliwa kwa wanaofikiriwa ni watovu wa nidhamu, utaratibu huo ufanyike wakiendelea na masomo yao.
Alisema wanaamini kurudi kwa wanafunzi hao, hakutazuia wala kukataza hatua hizo kuchukuliwa na kusisitiza kuwa nia yao si kutaka hatua za kinidhamu zisichukuliwe, lakini akasisitiza kuwa utaratibu bora ufuatwe ili haki na maridhiano ya kweli yapatikane kwa faida ya pande zote husika.
Loisulie alisema kwa kiasi kikubwa serikali haikujipanga sawasawa katika kushughulikia tatizo husika na kwa vyovyote vile ndio chanzo cha mgogoro. “Hii ilidhihirishwa na kauli kinzani za serikali kupitia Waziri wa Elimu ambapo awali alikubaliana na maamuzi ya TCU (Tume ya Vyuo Vikuu), lakini baadaye akabadili kauli kuwa serikali itatoa pesa kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo. Hali kama hii imelazimu kutokea kwa migogoro katika taasisi hii ya elimu ya juu. Wanafunzi ni waathirika tu wa tukio zima,” alisema Loisulie.