Umoja wa mataifa umelenga kutangaza kuwa sehemu kadhaa nchini Somalia zinakabaliwa na janga la kimataifa kufuatia ukame na njaa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa hali ya ukame inayoshuhudiwa nchini Somalia ni mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 50.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema kuwa mashirika ya kutoa misaada yanahitaji kupata hakikisho zaidi kutoka makundi ya wapiganaji hasaa wale wa Al shabaab kabla kupeleka misaada nchini humo.
Kundi la Al shabaab ambalo lina uhusiano na lile la magaidi la Al Qaeda lilikuwa limewekea mashirika hayo marufuku ya kufanya kazi katika maeneo ya kusini mwa Somalia. Hata hivyo marufuku hiyo iliondolewa wiki iliopita.
Na shirika la Oxfam limelalamika kuwa wafadhili wamelegea katika kuchangia misaada kusaidia walioathirika na ukame katika upembe wa Afrika.
Shirika hilo limesema kati ya dola bilioni moja zinazohitajika, kufikia sasa ni dola milioni 200 zilizokusanywa kufikia sasa.
Shirika hilo limewataka wafadhili waitikie mwito huo kwa haraka kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.
Huku, harakati za kuwashawishi wafadhili watoe michango yao, raia wa Somalia wanaofanya biashara nchini Kenya na ng'ambo, wameanzisha juhudi za kuchangisha pesa na vyakula kusaidia wenzao.
Ingawa mwenyekiti wa kundi hilo Hassan Guled hajaweka bayana wamechangisha kiwango kipi cha pesa na ni misaada kiasi kipi imekusanywa amesema mikakati inafanywa kuanza kusafirisha vitu vilivyopatikana hadi kwenye mpaka wa Kenya na Somalia walipo wakimbizi hao.
0 Comments