KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’, Charles Boniphace ‘Mkwasa’ amesema hahofii timu yake kupangwa na vigogo katika michezo ya Afrika itakayofanyika Septemba mwaka huu nchini Msumbiji.
Akizungumza na gazeti hili, Mkwasa alisema timu ilizopangwa nazo Twiga Stars zinajulikana na haoni sababu ya kuzihofia.
Julai 12 Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilipanga ratiba ya michuano hiyo, ambapo Tanzania ilipangwa Kundi B pamoja na Afrika Kusini, Zimbabwe na Ghana. Kundi A lina timu za Msumbiji, Cameroon, Guinea na Algeria.
Kwa upande wa wanaume Kundi A lina nchi za Msumbiji, Afrika Kusini, Libya na Madagascar, huku Kundi B likiwa na Cameroon, Uganda, Ghana na Senegal Michuano ya All Africa Games imepangwa kufanyika Maputo, Msumbiji kuanzia Septemba 3 hadi Septemba 18 mwaka huu.
Afrika Kusini na Msumbiji ni miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zikiisumbua Twiga Stars karibu kila mara zinapokutana na haijawahi kuibuka na ushindi katika mechi ilizocheza nazo.
“Afrika Kusini na Zimbabwe zote nazifahamu, tumeshakutana nazo mara nyingi, hatuna haja ya kuzihofia na hata wiki iliyopita tulicheza na Zimbabwe wakatufunga kwa penalti.
“Afrika Kusini nao tulikutana nao fainali za Afrika mwaka jana kwao wakatufunga kwa tabu bao 1-0, hivyo jambo la msingi ni kufanya maandalizi ya nguvu mapema, ni kundi la kawaida,” alisema Mkwasa.
Twiga Stars ilirejea Dar es Salaam Jumatatu ikitokea Harare, Zimbabwe ilikoshiriki michuano ya Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) ikiwa timu mwalikwa, ambapo timu nane zilishiriki wakiwemo wenyeji Zimbabwe.
Nyingine zilikuwa ni Lesotho, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi, ambapo Twiga ilishika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.
1 Comments
Nice Article, clear and detailed description...
Thanks a lot for sharing the information.....
By the way check the latest information about the All Africa Games 2011 here, like events, programs from All Africa Games 2011.