Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki na Demokrasia nchini, Denis Maringo, amesema pamoja na sheria ya utafiti na uchimbaji wa mafuta nchini kutimiza miaka 20, sekta hiyo bado haijaweza kuwaletea unafuu wa maisha wananchi wanaoishi katika maeneo ya tafiti za mafuta na gesi na nchi kwa jumla.
Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na athari za kimaendeleo wanazopata wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Maringo alisema pamoja na sheria hiyo kutimiza miaka 20, bado nchi haijawa na mpango mkakati wa mazingira wa kitaifa, ambao utafuatwa na makampuni yanayokuja kufanya utafiti na kuchimba madini.
Alisema hali hiyo inasababisha makampuni hayo kuendesha tafiti na uchimbaji wa gesi bila mwongozo wa nchi.
“Na ndiyo maana kuna uharibifu mkubwa sana wa kimazingira unaoendelea kwenye maeneo ya pwani, ambako kunafanyika tafiti hizo. Hivi sasa kuna makampuni zaidi ya 20 yanayoendesha tafiti za mafuta na gesi nchini. Dalili kwamba kuna mafuta tayari, sasa tusipokuwa na mwongozo, hali inayotokea kwenye migodi ya dhahabu itatokea na kwenye mafuta na gesi vilevile,” alisema.
Alisema kwa mfano pamoja na gesi kuchimbwa kwa muda sasa, bado haijaweza kutatua tatizo la umeme lililopo nchini na kwamba, hata mikataba pia imegubikwa na usiri mkubwa unaozuia wananchi kuelewa kilichoandikwa.