MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto, ameunda kamati ndogo ya uchunguzi wa sakata la uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Kamati hiyo iliyopewa siku 14 kumaliza kazi yake na kutoa ripoti, imeundwa na wabunge saba, akiwamo wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), ambaye anawakilisha wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Wengine ni Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), wa Viti Maalumu, Amina Mwidau (CUF) na wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM).

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Angelah Kairuki (CCM) na wa Muheza, Herbet
Mtangi (CCM).

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jana, Zitto alisema kamati yake, imemwandikia Spika barua ikimwomba kuidhinisha mapendekezo ya wabunge watakaounda kamati hiyo ndogo ili kuchunguza sakata zima la uuzwaji wa UDA.

Alisema, kamati hiyo itaanza kazi baada ya Spika kuridhia na ili kazi ya uchunguzi ifanikiwe, amewasilisha pia ombi kwa Spika kuomba Serikali iwasimamishe kazi watuhumiwa wote ambao bado wako kwenye sakata hilo, ili kupisha uchunguzi.

Hadidu za rejea za kamati hiyo ndogo ni pamoja na kuchunguza kama utaratibu wote wa kisheria ulifuatwa wakati wa kuibinafsisha UDA.

Nyingine ni kuchunguza kama Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), walitimiza wajibu wao ipasavyo.

Vilevile kuwaita mbele ya kamati wadau wote wa UDA hususan Bodi ya UDA, iliyokuwepo, Meya wa Jiji hilo, Mkurugenzi na Mkurugenzi Mtendaji wa UDA.

Kamati hiyo ndogo pia itamhoji mmiliki wa Kampuni ya Simon Group, Msajili wa Hazina, Mkurugenzi wa CHC na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.

Kazi nyingine za kamati hiyo ndogo ni kufanya tathmini ya UDA katika mazingira ya sasa ya kibiashara ya usafirishaji jijini, kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuwa na makosa katika ubinafsishaji wa shirika hilo.

Kuhamishwa kwa mchakato wa uchunguzi wa suala hilo kutoka Kamati ya Miundombinu kwenda POAC, kumetokana na kukosekana kwa imani na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo.

Mmoja wa wajumbe wake ni Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya ambaye anadaiwa kumiliki hisa 10,000 za kampuni iliyoinunua UDA ya Simon Group.

Sakata la UDA liliibuka bungeni wakati wabunge wakichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Uchukuzi ya mwaka 2011/12 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.