KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ Jan Poulsen(pichani mwenye kofia) amekerwa na tabia ya utovu wa nidhamu iliyooneshwa na mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ ya kushindwa kuripoti katika kambi ya timu ya vijana ya chini ya miaka 23 iliyokuwemo jijini Arusha.
Poulsen aliwaita wachezaji watatu Gaudence Mwaikimba, Juma Seif ‘Kijiko’ na Boban kuja jijini Arusha kucheza michezo miwili ya kirafiki kati ya Vijana Stars na Shelisheli ili aangalie uwezo wao kama anaweza kuwaita katika kikosi cha Taifa Stars.
Haruna Moshi
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Poulsen alisema ni mchezaji mmoja tu aliyeitikia mwito huo ambaye ni Kijiko, huku Mwaikimba akitoa taarifa kuwa ni mgonjwa lakini Boban hakukuwa na taarifa zozote juu yake.
Kocha huyo raia wa Denmark alisema, wakati wanaondoka Dar es Salaam mchezaji huyo alisema atakuja na usafiri wake binafsi lakini hadi sasa haijulikani alipo.
“Sijawahi kumwona Boban akicheza lakini niliambiwa ni mzuri na pia niliambiwa kuwa ni mchezaji ambaye hana nidhamu na kweli nimeliona hilo mwenyewe,”alisema.
Kocha huyo alisema kutokana na hali hiyo yeye atapeleka ripoti kwa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambayo itaamua hatua za kuchukua dhidi ya Boban.
Akiizungumzia Vijana Stars, Poulsen alisema, kuna wachezaji watano wa timu hiyo wanastahili kujiunga na timu ya wakubwa ya Taifa Stars kwani wameonesha uwezo mkubwa kiuchezaji.
Alisema mbali ya hao hata Kijiko naye ameonesha kiwango kinachostahili hivyo naye yuko katika mipango yake ya baadaye.
Awali, kocha huyo ilikuwa atangaze kikosi cha Stars kitakachocheza mechi ya kimataifa ya rafiki, lakini alishindwa kufanya hivyo baada ya mechi hiyo kuahirishwa.
Hivyo, kutokana na hilo, sasa timu hiyo itatangazwa baadaye itakapopatikana timu ya kucheza nayo mechi ya kirafiki.
Ofisa abari wa TFF, Bonface Wambura alisema, baada ya kukosekana kwa mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Palestina sasa Shirikisho lake lipo mbioni kutafuta mchezo mwingine wa tarehe hiyo hiyo Fifa, Agosti 10.
Alisema wanafikiria kuomba kucheza na timu za taifa za Malawi na Botswana.Wambura alisema awali nchi hizo zilikubali kucheza na Stars lakini wao waliamua kutaka kucheza na Palestina hivyo watarudi tena kukumbusha juu ya hilo na kuna uwezekano mkubwa hilo kufanikiwa.
0 Comments