AFYA ya kondoo wa ajabu aliyezaliwa katika Kijiji cha Uduru wilayani Hai mkoani Kilimanjaro iko shakani kutokana na mazingira yasiyo salama anakoishi.

Bwana Mifugo wa vijiji vya Uduru na Nkuu Andrea Njau amesema jana kuwa kondoo huyo yupo katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa magonjwa yanayotishia maisha yake.

“Kondoo huyo yupo katika mazingira ambayo hayastahili hata kidogo, magonjwa kama ya homa ya mapafu, ndigana baridi, kimeta pamoja na fangasi yatakuwa yakimnyemelea,” alisema Njau.

Njau alisema tangu aanze kuhudumia mifugo katika kijiji hicho, hajawahi kutoa tiba wala chanjo katika familia ya mmliki wa kondoo huyo, Grace Masawe hali inayotishia zaidi maisha ya kiumbe huyo.



Akifafanua sababu na dalili za magonjwa hayo yanayopatikana katika kijiji hicho, Njau alisema kuwa homa ya mapafu ambayo husababishwa na minyoo ya mapafu, mfugo huwa na homa kali na hutoa mapovu mdomoni na hatimaye kufa.

Kuhusu ugonjwa wa ndigana baridi, Njau alisema husababishwa na kupe wanaozaliana kwa wingi kutokana na kinyesi cha ng'ombe na kuonya kuwa kama kondoo huyo anakaa zizi moja na ng’ombe, yuko hatarini kuupata.

Ugonjwa mwingine hatari unaomnyemelea kondoo huyo ni kimeta (anthrax) ambao huua
mifugo ghafla pamoja na binadamu.

Alisema ugonjwa huo uliwahi kuzuka hivi karibuni katika eneo hilo lakini ulidhibitiwa kwa
haraka kabla ya kuleta madhara makubwa.

Ugonjwa wa kimeta hauna dawa yoyote zaidi ya chanjo ambayo katika Wilaya ya Hai mwanzoni mwa Juni chanjo hiyo ilitolewa.

Alisema mbali na kutowahi kuhudumia mifugo ya familia ya Masawe, lakini hata wakati wa chanjo dhidi ya kimeta, wafugaji wachache walitoa mifugo yao kutokana na kukosa elimu.

Masawe alikiri kuwa hajawahi kupatia mifugo yake chanjo ya aina yoyote hata na kondoo huyo kwa madai kuwa hana fedha ya kuwapatia matibabu.

Mmiliki huyo alisema kuwa katika mifugo yake ulishawahi kuzuka ugonjwa ambao hakuutambua ukaua ng'ombe wake ghafla.

Kutokana na hali hiyo, Njau alishauri jamii ijitokeze kumsaidia mama huyo ili amlinde kondoo huyo dhidi ya hatari ya magonjwa.

Kondoo huyo dume alizaliwa Julai 6 mwaka huu, akiwa na maandishi ya Kiarabu ubavuni yenye maana ya neno Yasini ambayo ni aya muhimu sawa na moyo wa Kitabu Kitakatifu cha
Koran.

Tangu aripotiwe na gazeti hili, kondoo huyo amekuwa kivutio kikubwa kwa watu hususani waumini wa dini ya Kiislamu wanaomiminika kwa wingi kutoka mikoa mbalimbali kushuhudia maajabu hayo.

Waumini hao baadhi wamefikia hatua ya kutaka kumnunua kwa Sh milioni 10 lakini wakakataliwa na mmiliki huku baadhi ya mashehe wakisema ni dalili za kiama.

Tayari Baraza la Waislamu Mkoa wa Kilimanjaro limeshatoa maelezo kuwa kondoo huyo ni jambo kubwa na hivyo wanamuachia Mungu.