KAMPUNI ya Commercial Petroleum (COPEC) ambayo imepewa leseni na Serikali kuagiza bidhaa ya petroli, imeahidi kuingiza nchini shehena yake ya kwanza ya mafuta mwishoni mwa mwezi ujao.

Tayari kampuni hiyo tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetangaza zabuni ikialika wafanyabiashara ambao wako tayari kusambaza bidhaa itakayoagizwa nayo.

Copec ilipewa leseni juzi na Serikali baada ya waagizaji binafsi wa petroli kugoma kutokana na Serikali kutangaza bei elekezi chini ya waliyokuwa wanauzia.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Selengia Mlawi, aliliambia gazeti hili jana, kuwa Serikali imekubali kuipa kampuni hiyo dola milioni 38 za Marekani, kwa ajili ya kuagizia shehena yake ya kwanza.

Imetoa fedha hizo kutokana na dharura iliyopo, baada ya wafanyabiashara binafsi kugoma kusambaza mafuta hayo.

TPDC ilikiri kuwa kwenye mipango yake, suala hilo halikuwamo na ndiyo maana Serikali ikaamua kutoa kiasi hicho cha fedha, ambacho kinatosha kununulia, kusafirishia na kulipia bima shehena yake ya kwanza.

Lengo la Serikali kuruhusu kampuni hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na TPDC kujiingiza kwenye biashara ya ushindani, ni kujaribu kupata taarifa sahihi na za uhakika kuhusu uagizaji wa bidhaa hiyo, kutokana na wafanyabiashara binafsi kulalamika kuwa wanapata hasara.

Lingine, ni kuhakikisha kinakuwapo chombo cha uhakika ambacho hakiwezi kupinga wala kutofautiana na maagizo ya Serikali, kama walivyofanya waagizaji binafsi, hadi wakagoma kusambaza bidhaa ya petroli na hivyo kuiingiza nchi kwenye janga la uhaba wa mafuta.

Serikali ina ubia na kampuni ya BP kwa asilimia 50, lakini kampuni hiyo ndiyo inaonekana kushikilia msimamo wa kuendelea na mgomo licha ya agizo la Serikali kukataza mgomo huo.

Hata hivyo, COPEC imeingizwa kwenye biashara hiyo wakati haina watendaji wala bodi, jambo ambalo limeifanya TPDC katika kipindi cha mpito, kuchukua majukumu makubwa ambayo yangeendeshwa na bodi na menejimenti ya Copec.

“Ni kweli, kwa sasa kampuni haina watendaji, kikao cha Bodi cha TPDC kilikaa juzi (Jumanne) na kuamuru wafanyakazi walioko kwenye kitengo cha masoko cha TPDC waendeshe shughuli za kampuni hiyo wakati menejimenti yake ikitafutwa,” alisema Mlawi.

Mlawi alisema pia kwamba Bodi ya TPDC chini ya uenyekiti wa Jenerali (mstaafu) Robert Mboma, ndiyo itakayounda bodi ya COPEC na ilikubaliwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya TPDC waingie kwenye bodi hiyo, ili kuipa uhai na kasi ya kuendesha biashara hiyo.

Ndiyo maana hata tangazo la jana la kukaribisha zabuni ya kusambaza shehena ya COPEC lilitolewa na Bodi ya TPDC kwa niaba ya mpuni hiyo.

Katika tangazo hilo, zabuni inawataka wenye sifa za kusambaza tani 9,000 za petroli, 25,000 za dizeli na tani 1,000 za mafuta ya taa. Mwisho wa kuomba zabuni hiyo ni Septemba 12.

“Shehena ya kwanza kuwasili nchini haitazidi mwisho wa Septemba, hivi sasa tunajiandaa kupeleka zabuni kwenye kampuni kubwa ili zituuzie mafuta kwa bei ndogo zaidi kuliko kununua mafuta kutoka meli zinazoelea baharini.

“Sisi tunaingia kwenye mfumo wa zabuni, si kuagiza kwenye kampuni mama kama wanavyofanya BP na Engen, ambao wanapewa bei kabisa na ndiyo maana inakuwa vigumu kwao kubadilisha bei, kwani ni lazima wapate kibali cha kampuni hizo mama,” alisema Mlawi.

Akifafanua kuhusu wafanyakazi, alisema TPDC tangu mwaka 2006 imekuwa na wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya mafuta, kwani tayari Serikali iliwaomba kufanya biashara hiyo na baadaye wakasimamisha suala hilo.

“Tayari tulishaajiri wataalamu kutoka kampuni za mafuta … na uhakikishia kuwa hilo halina shida kwa vile tunao wa kutosha katika kitengo cha masoko,“ alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Maghala Mlawi alikiri kuwa kwa sasa hawana maghala ya kuhifadhia shehena watakayoagiza lakini akasema biashara ya mafuta inaruhusu kampuni kutumia maghala ya kampuni nyingine.

“Kwa kipindi hiki ambacho hatuna maghala, tutaomba kampuni nyingine, kwani sheria inaruhusu kampuni shindani kutupa maghala hayo hata kama tuna ugomvi nao. Kwa hivyo hatuna tatizo na suala hilo,” alisema Mlawi.

Pia alisema wataangalia uwezekano wa kutumia maghala ya kampuni ya kusafisha mafuta ya Tiper, kwani ina maghala ya kutosha kuhifadhia shehena za mafuta.

Alisema kitendo cha COPEC kuingia kwenye biashara hiyo ya ushindani kutawafanya wafanyabiashara binafsi kutoichezea tena Serikali.

Alisema ana uhakika wataendesha biashara hiyo vizuri, licha ya vita vya kutaka kuwakwamisha ili wasiingie katika biashara hiyo.

Vita serikalini Kampuni hiyo licha ya kuanzishwa mwaka 1999, Serikali iligoma kuipa leseni ya biashara hiyo, hali inayoelezwa na baadhi ya vyanzo vya habari kutoka ndani ya TPDC, kuwa ulikuwa ni mpango uliohusisha baadhi ya maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini.

Hali hiyo iliifanya TPDC kushindwa kuunda menejimenti yake. Vita dhidi ya COPEC viliifanya Serikali iiamuru TPDC kuachana na biashara ya mafuta badala yake ijielekeze kwenye kutafuta na kutafiti mafuta.

Mwaka 2006 kampuni hiyo ilifufuliwa baada ya kutokea uhaba wa mafuta, lakini baadaye Serikali ikaitaka isiendelee na mpango wake wa kuagiza mafuta.

Baada ya kutokea tena uhaba wa mafuta juzi kutokana na mgomo wa wafanyabiashara binafsi, Serikali katika kikao chake kilichohusisha watendaji wa Ikulu, Wizara ya Nishati na
Madini, TPDC na Ewura, iliamua COPEC iingie rasmi kwenye biashara ya ushindani wa mafuta.

Mpango wa baadaye Kwa mujibu Mlawi, licha ya kupewa kiasi hicho na Serikali, itaendelea sasa na mpango mkakati wake wa kujiimarisha kibiashara, ikiwa ni pamoja na kukopa fedha kutoka vyanzo vya ndani ili iweze kujiingiza kwenye ushindani zaidi.

Alisema pia fedha watakazopata licha ya kuzitumia kuagizia shehena ya mafuta, watazitumia kujenga vituo ya kusambazia mafuta na maghala.

“Tumefanya biashara hii ya mafuta muda mrefu tunaifahamu nakuhakikishia kuwa pamoja na kuungwa mkono na Serikali, lakini tutatoa ushindani wa kutosha,” alisema Mlawi.

Vituoni jana Upatikanaji wa bidhaa ya petroli katika vituo vya mafuta ulikuwa wa kusuasua, kwani vingi havikuwa na bidhaa hiyo, licha ya kampuni kubwa kuruhusu kusambazwa.

Kutokana na mahitaji kuwa makubwa, vituo vingine viliuza nishati hiyo juzi jioni na kujikuta vinaishiwa, hivyo kulazimika kusimamisha huduma na kufanya wananchi waendelee kuhangaika.

Vituo vya BP na Engen pia viliendelea kutotoa huduma hiyo kutokana na maghala ya yake juzi kutoruhusu kusambazwa kwa shehena yake.

Naye Halima Mlacha, anaripoti kwamba wakati hali ya uuzaji mafuta ikiendelea kutengemaa sehemu mbalimbali nchini, bado baadhi ya wasambazaji wa mafuta hayo hasa wa BP walionekana dhahiri kutouza mafuta hayo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye maeneo kadhaa ya Dar es Salaam ulishuhudia vituo kadhaa vya mafuta vya BP na CamelOil vikiwa haviuzi mafuta, huku wafanyakazi wao wakionekana kupiga soga.

Vituo vya BP vya Mwenge, Mikocheni, Sinza Kijiweni, Ocean Road na Kinondoni, vilikuwa tupu, bila dalili zozote za biashara.

Hali ilikuwa vivyo hivyo katika vituo vya CamelOil Afrika Sana, Engen Mikocheni na OilCom. Hata hivyo, gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vituo vya TSN Oil Bamaga, GBP na Big Bon Afrika Sana, vikiendelea na biashara ya mafuta ambapo kwa jana hakukuwa na foleni kubwa ya magari na watu kama ilivyokuwa juzi.

Vituo vingine vilivyokuwa vikiuza mafuta ni Oil Com Mwananyamala, Gapco na Oryx Posta Mpya.

Mfanyabiashara maarufu nchini na msafirishaji mizigo nje ya nchi, Azim Dewji, alitupia
lawama Ewura na Serikali kwa tatizo hilo la ukosefu wa mafuta na kuhadharisha juu ya kurejea enzi za kupanga mistari kununua bidhaa kama sabuni.

“Wanataka kuturejesha enzi za foleni, hii si sahihi kabisa, nchi ilikuwa inakabiliwa na tatizo la umeme, sasa imeibuka la mafuta, ambalo linatokana na kuchanganya siasa na biashara, tunaomba Serikali iliangalie vizuri suala hilo,” alisema Dewji.

Alisema tatizo linaloendelea limetokana na Ewura kulazimisha wafanyabiashara kuuza mafuta chini ya gharama zao za uendeshaji, hali ambayo alidai inatokana na biashara kuchanganywa na siasa.

“Jamani ikumbukwe kuwa bei ya mafuta inadhibitiwa na soko la dunia, hakuna mfanyabiashara mwendawazimu anayenunua mafuta halafu akae nayo,” alisema.

Aliitaka Ewura iweke wazi vipengele ambavyo Serikali imefuta ushuru ili vibainike, kwa kuwa sasa jambo hilo bado ni siri, hali inayosababisha shaka kuwa hakuna punguzo lililofanyika.

Akizungumza na HABARILEO, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema kuhusu baadhi ya vituo kutouza mafuta Bodi ya Mamlaka hiyo inatarajiwa kukutana leo, pamoja na mambo mengine, kujadili suala hilo na hatua za kuchukuliwa.

Kuhusu kutoweka wazi vipengele vya ushuru uliopunguzwa na Serikali, alisema suala hilo si la kweli na kwamba hata katika ukokotoaji wa bei hizo mpya, kila kipengele kilioneshwa na kampuni zote za biashara kupewa nakala.