Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga akilizungumza Baraza Kuu la  Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya Video Teleconference kutokea Mogadishu. katika taarifa yake kwa Baraza hilo ambalo lilikutana siku ya Jumatano, Mahiga amesema,  wananchi wa  Somalia na ambao wanakabiliwa na  baa kubwa la njaa na ukame hawawezi kusubiri zaidi. Na akalitaka  Baraza hilo kuzihimiza  serikali mbalimbali kutoa misaada ya kibinadamu haraka  ili kuokoa maisha ya watu na hasa watoto wadogo. Na Mwandishi MaalumNew York


Balozi Augustine Mahiga, Mwakilishi Maalum wa Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia,  ameliambia Baraza Kuu la Usalama kwamba  wananchi wa Somalia ambao wanakabiliwa na   baa  la njaa na ukame hawezi  kuendelea kusibiri.

Na kwa sababu hiyo, Mahiga amewataka wajumbe wa Baraza hilo, kuzichagiza serikali zao  zichangie  kwa haraka na kwa kiwango cha kuridhisha misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya   wananchi wa Somalia.

Akizungumza kwa njia ya video teleconference kutokea  Mogadishu,  siku ya  jumatano. Mahiga anasema  zinahitajika dola  za kimarekani Bilioni Moja  ili kukabiliana na janga hilo la njaa na ukame.

Hata hivyo  anasema,  hadi wakati anazungumza na Baraza hilo, fedha au michango ambayo imekwisha tolewa na jumuia  ya kimataifa  ilikuwa  haijafikia hata nusu ya mahitajio halisi.

“ Ninawaomba nyie wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama, mzihamasishe serikali zenu zichangie kwa haraka na kuokoa maisha ya wasomali. Kwa ujumla niseme wasomali hawawezi kuendelea kusubiri zaidi” akasema Mahiga.

Balozi Mahiga anasema hali ni ya kutisha, watu wanapoteza maisha kwa  idadi kubwa na hasa watoto wadogo.

Akizungumzia hali   ya kisiasa na kiusalama  na hasa baada ya wapiganaji wa Al Shabaab kuondoka  mjini Mogadishu. Mahiga anasema  kuondoka kwa kundi hilo  kumetoa fursa  lakini na    changamoto pia.

“Kuondoka kwao  kwa kweli ni mshango mkubwa kwetu sote. Na kumetoa changamoto na fursa pia. Fursa ya kwamba sasa  Serikali ya Mpito ( TFG)  kwa kushirikiana na   Vikosi ya Kulinda  Amani ( AMISOM)sasa wanashikilia asilimia 95 ya mji wa Mogadishu kwa mara ya kwanza. Changamoto ni namna ya kuendelea kuyashikilia maeneo hayo yaliyoachwa na kundi hilo”.  anasisitiza Mahiga.

Anasema, kwa kuimarisha  eneo lililoachwa na Al Shabaab kutasaida pia katika kulizuia kundi hilo lisireje tena katika  maeneo ambako limeondoka.

Akabainisha kuwa baada ya kundi hilo kurudi nyuma na kutokomea katika maeneo tofauti na likiwa limegawanyika katika mkundi mawili, kumeongeza kasi ya usambazaji wa misaada ya kibanadamu kwa waathirika.

Na kwamba  wananchi wengi waliokuwa wakiishi maeneo yaliyokuwa  yakishikiliwa na kundi hilo, sasa wanakimbili mjini Mogadishu kutafuta chakula.

Akasema  Ofisi ya kisiasa ambayo pia iko chini yake inaendelea kujipanga kwa kufanya tathmini na uchambuzi wa mahitaji halisi ambayo siyo tu yataviwezesha  AMISOM na TFG   kukalia  maeneo yaliyoachwa na Al-Shabaab , bali kuchukua maeneo mengine zaidi na hivyo kupanua wigo wake.

Wakati huo huo Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Bi Susan Rice amesema serikali yake inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na  Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia, Balozi  Augustine Mahiga.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa Baraza Kuu.  Susan Rice anasema serikali yake imekuwa ikifuatilia  kwa karibu kazi nzuri  na kubwa inayofanywa na Balozi Mahiga nchini Somalia .  Pamoja na  vikosi  vya kulinda amani vya Afrika  na kwamba inaunga mkono kila hatua ya juhudi hizo.

Akabainisha kuwa Marekani,  nchi ambayo kwa sasa ndiyo inayoongoza kwa kutoka misaada katika Pembe  ya Afrika.Itaendelea kuchangia kwa hali na mali  ikiwamo misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa  Somalia. Pamoja na  jitihada za kurejesha amani ya kudumu katika taifa hilo.