Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika linaloshughulikia maslahi ya watoto la UNICEF karibu theluthi moja ya watoto wa kike nchini Tanzania wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na kuingiliwa bila hiari kabla hawajatimia umri wa miaka 18.
Shirika hilo linasema kuwa watoto wa kiume idadi yao inafika asili mia 13.4.
Kinachotumika sana katika unyanyasaji huu ni kuwatomasa watoto ambako baadae hufuatiwa na jaribio lakutaka kuwaingilia.
Afisa mmoja wa shirika hilo Andy Brooks amesema uchunguzi huu ndio uliokamilika zaidi na umeonesha kuwa serikali iko tayari kukabiliana na tatizo hili.
Uchunguzi huu pia uligundua kuwa wale ambao wamejihusisha na mapenzi kabla ya kutimia umri wa miaka 18, asili mia 29.1 ya watoto wa kike na asili mia 17.5 ya wale wa kiume wamesema kuwa mara ya kwanza wao kujihusisha na ngono haikuwa kwa hiari yao.
Unicef inasema hii ina maana walilazimishwa ama kushawishiwa kujihusisha na ngono.
Waziri wa Elimu wa Tanzania Shukuru Kawambwa amesema kuwa serikali imejitolea kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na kuingiliwa watoto.
Bw Brooks amesema uchunguzi sawa na huo utafanywa nchini Kenya, Rwanda, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.