KITUO cha kujaza gesi kwenye magari kilichopo Ubungo, Dar es Salaam kina uwezo wa kujaza magari 200 kwa siku, Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, amewaeleza wabunge kuwa, mpaka sasa mifumo ya magari 36 imebadilishwa ili yatumie gesi asili badala ya mafuta.
Kwa mujibu wa Malima, kasi ya kubadilisha mifumo hiyo ni ndogo kwa sababu ya gharama.
Ameyasema hayo leo bungeni mjini Dodoma wakati anajibu maswali ya Mbunge wa Muheza, Herbert Mtangi aliyetaka kufahamu Serikali inasema nini kuhusu utekelezaji wa mradi wa matumizi wa gesi kwa ajili ya magari nchini.
“Takribani zaidi ya shilingi milioni moja zinahitajika kubadilisha mfumo wa gari moja linalotumia mafuta ya petroli kutumia gesi asili…aidha kasi ndogo ya kazi za masoko zimepelekea ufahamu mdogo wa manufaa ya matumizi ya gesi kwenye magari ikilinganishwa na matumizi ya petroli” amesema Malima.
Malima amesema, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Pan African Energy walianza mchakato wa mradi wa kutumia gesi asili kwenye magari , viwandani, majumbani na matumizi mengine ya chanzo hicho cha nishati ili kupanua manufaa ya kiuchumi na kijamii.
0 Comments