BARAZA la Usalama la Taifa limeagiza iundwe haraka tume ya wataalamu kuchunguza kwa uwazi chanzo cha ajali ya mv Spice Islanders iliyoua watu 197 na wengine 619 kujeruhiwa Jumamosi.
Akitoa tamko la Baraza hilo katika dua ya kitaifa iliyosomwa Zanzibar jana na kutangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya elektroniki, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alisema matokeo ya uchunguzi huo yatatakiwa kuwa wazi ili kila mwananchi aelewe kilichotokea.
Pia mamlaka za udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini za pande zote za Muungano zifanye kazi kwa ushirikiano ili kudhibiti matukio kama hayo.
“Mamlaka hizo zinatakiwa kuwa na vigezo vinavyofanana vya kutoa hati za ubora wa usalama kwa vyombo vya usafiri wa majini ... meli zinazotumika katika bandari zote zisiwe na vigezo tofauti,” alisema Luhanjo ambaye alitakiwa na Rais Jakaya Kikwete kusoma tamko hilo.
Pia Baraza hilo lilitaka vyombo hivyo vya majini kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara na taarifa zitolewe wazi kwa umma.
Hali kadhalika, Baraza lilitoa pongezi kwa vyombo vya habari hususan televisheni ya Zanzibar kwa kutoa taarifa zilizowezesha wafiwa kutambua maiti wao na pia vyombo vyote vya habari kwa kutoa taarifa ya tukio hilo kitaifa na kimataifa.
Lakini pia Baraza lilitoa shukurani kwa wananchi wa Zanzibar kwa ustahimilivu wao na ushirikiano tangu ajali hiyo itokee.
Vyombo vya usalama viliagizwa na Baraza hilo kuendelea kutafuta maiti hata nje ya visiwa vya Unguja na Pemba na hata ndani ya meli yenyewe, ili maiti watakaopatikana wazikwe kwa heshima kama binadamu wengine.
Serikali kupitia Baraza hilo, ilitoa pongezi kwa Serikali ya Afrika Kusini kwa kujitolea wapiga mbizi ambao watasaidiana na Watanzania kutafuta miili zaidi.
Ili kutambua maiti ambao hawakutambuliwa katika siku zijazo, Baraza liliagiza uchunguzi wa vinasaba ufanyike kwa maiti hao, ili watakapojitokeza ndugu zao waoneshwe makaburi yao.
Kwa Serikali zote mbili, Baraza la Usalama lilitambua mchango wa serikali hizo hususan kamati za maafa za pande zote mbili na kuziagiza kuendelea na ushirikiano huo katika kukabiliana na matatizo kama hayo ya maafa.
Mapema Rais Kikwete alielezea kuridhishwa kwake na ushirikiano uliobainika kwa Serikali zote mbili katika kukabiliana na hali hiyo ya ajali.
“Hakika kweli sisi ni wamoja wa kweli, ni wa damu moja ... tumeweza hiki hakuna litakalotushinda,” alisema Kikwete ambaye alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange na IGP, Saidi Mwema kwa mawasiliano na hatua za haraka walizochukua.
Naye Shein alimpongeza Kikwete na Serikali ya Muungano kwa hatua zilizochukuliwa na kuonesha kuwa kweli Watanzania ni ndugu wa damu moja.
Alishukuru nchi zilizotoa salamu za pole ambazo alisema ni nyingi na pia kwa washirika wa maendeleo waliokuwa pamoja na Wazanzibari katika msiba huo mkubwa.
Pia alishukuru kampuni binafsi za meli, hoteli za kitalii, Polisi, JWTZ, Usalama wa Taifa, madaktari na wauguzi, wataalamu mbalimbali wa afya, wanafunzi wa afya Zanzibar, taasisi mbalimbali za SMZ, mashehe, waumini wa dini mbalimbali, ofisi ya Mufti, Ofisi ya Kadhi Mkuu, madereva waliosafirisha maiti na majeruhi.
Alitoa shukurani maalumu kwa Makamu wa Rais wote, wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Iddi na vyombo vya Dola kwa jinsi walivyoshughulikia suala hilo, lakini pia wanahabari wote na wamiliki wa vyombo vya habari kwa kutoa taarifa ambazo ziliwafaidisha wananchi.
Alisema tukio hili limedhihirisha umoja, ushirikiano na mapenzi yaliyopo baina ya Watanzania wote kwani walionesha mshikamano wa hali ya juu.
Nayo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje imeanza kazi ya kuwahoji watendaji wakuu wa taasisi za bandari ikiwemo msajili na kuhoji kwa nini meli zinazosafiri Pemba hufanya safari zake katika nyakati za usiku.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowasa alitaka kujua kwa nini safari za meli zinazokwenda Pemba hufanyika katika nyakati za usiku ambapo ni vigumu sana kuweza kutoa huduma za uokoji wakati inapotokea ajali.
“Tunataka kujua kwa nini meli zinazokwenda Kisiwa cha Pemba hufanya safari zake katika nyakati za usiku....nyakati za usiku ni vigumu sana kutoa huduma za msaada wakati inapotokea ajali kama ilivyotokea kwa ajali ya meli ya Spice Islanders,” alihoji Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo walitaka kupatiwa jina la mmiliki wa meli hiyo na nani aliyetoa ruhusa ya kuondoka kwa meli hiyo wakati ilikuwa imejaa kupita uwezo wa idadi ya abiria wanaopaswa kuchukuliwa.
Mbunge wa Jimbo la Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahim Sanya ambaye alilazimika kutoa machozi ya huzuni kutokana na ajali hiyo, alitaka kupatiwa jina la mmiliki wa meli hiyo.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali wakati alipoulizwa nani mmiliki wa meli hiyo na Kamati ya Ulinzi alishindwa kutoa jibu na kusema ni taasisi ya bandari ndiyo inayofahamu jina la mmiliki huyo.
Hata Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud wakati alipozungumza na waandishi wa habari alikataa kutaja jina la mmiliki wa meli hiyo na kusema mamlaka za bandari ndiyo zinazofahamu jina lake.
Ujumbe huo ukiongozwa na Edward Lowassa pamoja na Makamu wake, Mussa Zungu na wajumbe wengine walisikitishwa na ajali hiyo na kusema uzembe umechangia kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, wakati ujumbe huo ukionana na watendaji wakuu wa Shirika la Bandari akiwemo Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari, Mustafa Aboud Jumbe na Msajili wa meli, waandishi wa habari walizuiliwa.
Hata hivyo, waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia katika kikao hicho muhimu ambacho kilikuwa kikiwahusisha watu muhimu wanaoshughulikia usafiri wa meli na kutoa ruhusa ya kuondoka kwa vyombo vya habari.
Mapema ujumbe huo ulipata nafasi ya kuonana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein huko nyumbani kwake Migombani na kutoa pole kutokana na ajali hiyo ambayo imeleta maafa makubwa kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Ujumbe huo ulipata nafasi ya kuwaona watu mbalimbali waliopatwa na mkasa huo, ikiwemo familia zilizopoteza zaidi ya watoto watano huko Mwanakwerekwe pamoja na Amani.
Mfanyakazi mmoja katika kitengo cha usalama ambaye hakutaka kutaja jina lake alikiri na kusema baadhi ya watendaji walitofautiana kuhusu hali ya meli na wengine kutaka kuzuia kuondoshwa kwa meli hiyo.
“Tulitofautiana baadhi ya watendaji....wengine tulisema meli isiondoke kwa sababu imejaa kupita uwezo huku huku ikionekana kuinama hata kabla ya safari,” alisema mfanyakazi huyo ambaye alikuwepo wakati meli ikiondoka.
Lakini alisema baadhi ya watendaji waliogopa na kuruhusu kuondoka kwa meli hiyo na kuanza safari zake kwenda Pemba kwa sababu wamiliki wa meli hiyo ni wafanyabiashara wakubwa.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amepongeza ujasiri na mshikamano mkubwa ulioneshwa na vikosi vya ulinzi na usalama, madaktari na wananchi wa Zanzibar katika kuokoa maisha ya watu baada ya kutokea ajali ya meli ya Spice Islanders usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Maalim Seif aliyasema hayo jana alipokuwa na mazungumzo na ujumbe wa viongozi wa CHADEMA ulioongoza na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, huko nyumbani kwake, Maisara mjini Zanzibar.
“Serikali ilifanya kazi ya ziada, wananchi walikuwa na nidhamu na utulivu wa hali ya juu, askari nao walifanya kazi nzuri sana na hata mabalozi na viongozi wote kwa jumla waliweza kushiriki kikamilifu na kutoa mchango wao baada ya kutokea maafa haya,” alisema Maalim Seif.
Makamo wa Kwanza wa Rais amesema tukio la ajali ya meli hiyo linatukumbusha wajibu wa Taifa kujiandaa na kuhakikisha linaondokana na kasoro zote zinazoweza kusababisha kutoka kwa maafa ya aina hiyo ambapo roho za watu wengi zimepota.
Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alisema maafa yaliyosababishwa na kuzama kwa meli hiyo yamewagusa Watanzania wote na ndio maana viongozi wa chama chake wameamua kuwapa pole kwa yaliyotokea na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa maisha ya abiria na kuwahudumia waliopoteza maisha.
Mbowe alisema kuna haja kianzishwe kikosi maalumu cha uokoji wa baharini ili kutoa huduma za haraka na za uhakika mara inapojitokeza haja kama hiyo.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), limetuma salamu za pole kwa Watanzania wote kutokana na ajali ya meli hiyo ya Spice Islanders.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shabani Simba ilisema kwa niaba ya Baraza na Waislamu wote kwa ujumla namuomba Allah (S.w) awape moyo wa subra na uvumilivu wafiwa.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu ametoa salamu za rambi rambi kwa ndugu jamaa na marafiki kutokana na vifo vya watu zaidi ya 200 vilivyotokana na ajali ya kuzama kwa meli hiyo.
“Wizara imepokea taarifa hii kwa masikitiko makubwa na inawapa pole wafiwa wote pamoja na kuwaombea afya njema wale wote walionusurika katika ajali hii. Tunamwomba Mwenyezi Mungu awafariji katika kipindi hiki kigumu,” alisema Nundu.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki-Moon, amemtumia salamu za rambirambi Rais Jakaya Kikwete, kutokana na ajali ya kuzama kwa meli hiyo.
Katika salamu zake, Katibu Mkuu amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuzama kwa kivuko hicho katika pwani ya Zanzibar na kwamba Umoja wa Mataifa uko pamoja wananchi wa Tanzania katika kipindi hiki kigumu.

0 Comments