POLISI mkoani Arusha wamemkamata Shabani Kiula (34), mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru mkoani Arusha, kwa tuhuma za kuingiza dawa za kulevya aina mbalimbali Gereza Kuu la Arusha.

Dawa hizo ni bangi zaidi ya kilo tano na ugoro bunda 10. Kiula alikamatwa na Askari Magereza wa gereza hilo baada ya kupata habari kutoka kwa raia wema juu ya uingizaji dawa hizo uliokithiri katika gereza hilo.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Akili Mpwapwa, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, Leonard Paul alisema kwa sasa mtuhumiwa yuko katika ulinzi wa polisi na uchunguzi zaidi unafanywa na ukikamilika atafikishwa kortini.

Hata hivyo, Leonard alikataa kusema kama uingizaji huo unashirikisha askari Magereza, lakini habari za uchunguzi zilizofanywa na gazeti hili zinasema baadhi ya askari wanahusika na biashara hiyo gerezani hapo.



Habari za uhakika kutoka gereza hilo zinasema kuwa Kiula alishafungwa miaka 30 kwa ujambazi wa kutumia silaha na alitoka kwa rufaa ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na wakati akiwa ndani, alikuwa akifanya biashara hiyo inayodaiwa ''kulipa ile mbaya'' na baadhi ya askari na wafungwa viranja.

Kiula inadaiwa huingiza dawa hizo kupitia genge la wafungwa wanaokwenda kulima nje ya gereza hilo na kazi hiyo ya kuingiza dawa hayo hupewa kiranja wa genge ambaye ni mfungwa ama askari magereza ambaye anakuwa anajua mchoro mzima wa askari siku hiyo ya uingizaji kupitia lango kuu la gereza hilo.

Vyanzo vya habari vilieleza kuwa kukamatwa kwa Kiula kunaweza kufanya baadhi ya askari kuzima kashfa hiyo kwani hakuna askari Magereza anayetaka siri hiyo kuwa wazi kwa sasa.


chanzo ni Habari Leo.