Abiria mmoja miongoni mwa walionusurika katika ajali ya meli MV Spice Islanders iliyotokea Nungwi, visiwani Zanzibar aitwaye Mbezi Wilbard Bilungi, 39, akisimulia namna tukio hilo la kusikitisha lilivyotokea na kusababisha kuzama kwa chombo hicho, alisema kwamba walianza kuona dalili za kifo tangu wakiwa katika bandari ya Malindi, mjini Unguja.
Bilungi, aliyeokolewa kimiujiza baada ya kuelea majini wakati akiwa miongoni mwa waliopigania roho zao kwa muda wa saa 7 wakielea majini mara baada ya kuanza kuzama usiku wa Ijumaa.
Alisema karibu abiria wote walipata mashaka kuhusu usalama wao na kuwalalamikia wenye meli kwamba maisha yao yako shakani lakini wafanyakazi hao waliwapuuzia .
Bilungi anasema kuwa, abiria waliwagomea wakaguzi wa tiketi wa meli hiyo waliokuwa wakiruhusu abiria kupanda melini na kuruhusu shehena kubwa ya mizigo. Mgomo huo ulilenga kuzuia meli hiyo isiondoke. Hata hivyo, abiria hao walitulizwa kwa kupunguzwa abiria 15 tu miongoni mwa mamia waliobahatika kupenya kwenye chombo hicho.
Bilungi, mkazi wa Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam anayefanya kazi katika kampuni ya Ujenzi ya China iitwayo Group Six, alikuwa akienda Pemba kikazi.
Akisimulia zaidi mkasa huo, alisema kuwa mgomo wa abiria waliokuwa wakilalamikia wingi wa abiria na mizigo melini ulidumu kwa muda dakika 20 tu kabla ya meli hiyo kung’oa nanga.
"Abiria tulianzisha mgomo tukigombana na wafanyakazi wa meli hiyo kutokana na hali ya msongamano mkubwa iliyokuwepo ndani. Hakukuwa na nafasi ya kusimama au kukaa.Mgomo huo ulisababisha meli hiyo kuchelewa kuondoka bandarini kwa dakika 20 zaidi ya muda wake," alisema.
Hata walipokuwa wakiondoka katika bandari ya Malindi, anasema kuwa meli hiyo ilikuwa ikienda polepole mno. Abiria karibu wote walikiwa kimya kila mmoja akiwa na mashaka ya pengine kitakachotokea. Mambo yalibadilika walipojikuta chombo hicho kikianza kusukwasukwa kwa mawimbi hali iliyokuwa kama inagonga kengele ya tahadhari kwamba kuna jambo la kutisha lipo njiani linakuja.
Hata hivyo, baadhi ya watu walikuwa na matumaini kuwa wangevuka salama katika rasi wa Nungwi kama ilivyozoeleka.
" Mambo yalizidi kuharibika baada ya kuanza kuona meli ikiwa inaimana kwa nyuma. Tulipochungulia wenzetu wa ghorofa ya chini ya meli walikuwa wakipigana kupanda kwenda juu ili kutafuta sehemu salama. Hapo ndipo tukazidi kupata hisia kwamba mambo si shwari," alisema.
Alifafanua kwamba, kitendo cha manahodha wa meli hiyo kutoka sehemu waliyokuwa wamekaa huku nyuso zao zikiwa na dalili zote za taharuki au kukata tama kwa kile wanachokifanya. Waliwaomba abiria watulie kabla ya kuchukua maamuzi mengine ya kutoa tangazo kwa njia ya vipaza sauti kwamba watu wayakimbilie mavazi ya kujiokolea maisha yao ( life jacket).
Mazingira hayo yaliamsha hisia za dhahiri kuwa hakuna usalama na kwamba yalikuwa maisha ya roho mkononi.
"Nilipowaona wakigombea life jacket, nami nikalichangamkia moja na kupanda juu ya meli hiyo kabla ya kuwashuhudia wenzangu wakiwa majini huku wakipiga kelele za kuomba msaada wa kuokolewa," alifafanua kwa huzuni.
Bilungi, alisema kwamba kufikia hatua hiyo katika mazingira hayo hakukuwa na jinsi zaidi ya kujirusha majini.
Baada ya kufika baharini, bahari ilikuwa imechafuka na hivyo mawimbi yalimsukasuka yakamzamisha na kumuibua wakati akipigania roho yake na kuwashuhudia baadhi ya akinamama na watoto wakimeza maji ya bahari kasha kutapatapa na kupoteza uhai wao.
" Nilijitahidi kuwang’ang’ania ili kuwaokoa wasichana wawili walioonekana kuwa kama ndugu wa familia moja.Niliwaomba na kuwaelekeza wazishikilie ndoo walizokuwa nazo. Hata hivyo, mmoja wao alishindwa kuhimili msukosuko huo mkubwa na kumshuhudia akipoteza uhai, jambo ambalo lilinitia simanzi sana ila sikuwa na jinsi. Yaani kushuhudia mtu akikata roho ambaye umejitahidi kumsaidia kwa uwezo wako wote lakini mazingira yamekunyima fursa ya kukamilisha na kufanikisha juhudi zako. Sitasahau tukio hili la aina yake," alisema.
Kwa muda wa saa saba mfululizo katika majira hayo ya usiku, wakisukwasukwa na upepo wa bahari huku wakikabiliwa na tishio la kifo, Bilungu aliendelea kuipigania roho yake kwa kushikilia vipande vya 'life jacket' lililochanwa na abiria wenzake waliokuwa wakiligombea ili kujaribu kujiokoa maisha yao.
Zilikuwa saa ngumu na za kutisha sana ambazo hujui nini kitatokea dakika yoyote ile huku ukishuhudia baadhi ya watu wakipoteza uhai kila baada ya muda fulani hadi walipokuja kuokolewa saa mbili asubuhi ya siku ya Jumamosi na boti ya Waitaliano.
"Tangu nilipotumbukia majini kwenye majira ya saa 6 hivi usiku. Nilikuwa baharini nakabiliana na mawimbi huku baridi kali ikituadhibu. Niliipigania roho yangu huku nikishuhudia wenzangu wakifa bila wokozi wowote. Niliendelea kuwa kuwa kwenye mazingira kati ya duniani na ahera nikiwa nimekata tama kabisa kasha kwa namna ya ajabu kabisa ndipo muujiza ukatokea kwa kuokolewa na boti ya Waitaliano," alifafanua.
Alisema vifo vingi vya wenzake vilichangiwa na kuchelewa kupatikana kwa huduma ya uokozi.
Abiria huyo, alisema kwamba hali ilizidi kuwa mbaya baada ya meli kubinuka kabisa na kumwaga baharini shehena ya mizigo ambayo iliwajeruhi baadhi ya waliokuwa majini akiwemo yeye aliyeumia miguuni.
Pia, alisema kuwa meli hiyo imezama ikiwa na watu wengi hasa akinamama na watoto, ambao hawakufanikiwa kutoka wakati wa ikizama baharini. Alioomba sana serikali iseme wazi badala ya kuficha ukweli wa mkasa huo wote.
"Watu walikuwa wengi mno katika meli hiyo. Yawezekana ilibeba zaidi ya watu 1,000 huku waathirika wakuu wakiwa ni akina mama na watoto ambao naamini walisalia ndani ya meli wakati ikibinuka na kuzama," alisema.
Alipoulizwa, alijisikiaje alipojikuta ni mmoja wa waliokoka katika ajali hiyo, Bilungi, alisema alimshukuru Mungu kwa kuwa kama uokoaji ungechelewa kwa zaidi ya nusu saa tu , angeviachia vipande vya sponji alivyovishikilia kwa sababu miguu na mwili wake ni kama ulikuwa umekufa ganzi kwa baridi kali ya baharini.
"Mwili wangu ulikufa ganzi, kiasi nilishakata tamaa na kuanza kufikiria kuviachia vipande vile ili roho yangu itwaliwe. Lakini wakati huo kumbe ndipo miujiza yake iliponitokea kwa kuokolewa na boti hiyo ambayo ndani yake kulikuwa na manusura wengine wanane ," alisema.
Alisema, baadae aliwaelekeza sehemu nyingine wenye boti hiyo kwenda kuwaokoa watu wengine wane akiwemo dada aliyempoteza mwenzake kwa kushindwa kuishikilia ndoo kabla ya kuingizwa kwenye meli za wokozi na kupelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja kupata huduma ya kwanza ili kuyaokoa maisha yake.
Bilungi, alisema ni lazima serikali iwachukulie hatua kali za kisheria walioruhusu meli hiyo kuzidisha idadi kubwa ya abiria na mizigo kinyume na uwezo wa meli.
“ Naamini kabisa kuwa, kama jambo hilo lisingefanyika abiria wangefika salama katika safari yao na maisha yangeendelea kinyume na ilivyotokea,” alifafanua.
Pia, alisema ni wajibu wa serikali kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kuepusha ajali nyingine, aliyodai inaweza kutokea wakati wowote visiwani humo, kutokana na kuwepo kwa usimamizi mbovu wa vyombo vya usafiri wa majini.
Alisema meli na boti zinazotumika kwa usafiri kati ya visiwa vya Pemba na Unguja ni chakavu na mbovu hata kwa kuziangalia kwa macho tu, lakini zimekuwa zikiachiwa kufanya shughuli zake, kitu alichodai ndio sababu ya maafa yanayotokea mara kwa mara katika usafiri huo visiwani humo.
Abiria huyo anasema katika mkasa huo, alipoteza simu zake mbili, kiasi kikubwa cha fedha na nyaraka zake muhimu katika tukio hilo.
Alisema kwa jinsi Mungualivyomtendea miujiza huo hana cha kumlipa zaidi ya kumshukuru na kujiangalia upya katika mfumo wa maisha yake.
"Naamini Mungu ameniponya kwa nia ya kunipa somo, hivyo licha ya kumshukuru, pia naahidi kumtumikia nikibadili mfumo wa maisha nilionao, " alisema.
Baada ya kunusurika katika janga hilo na kufanikiwa kurejea jijini Dar es Salaam, alipokewa kwa mapokezi makubwa ambayo hajawahi kufanyiwa. Mapokezi hayo yalijumuisha familia yake na majirani zake tukio lililompa faraja kwamba kumbe anapendwa, kuthaminiwa kutokana na kuishi kwa wema na wenzake.
CHANZO: NIPASHE
1 Comments