Wafungwa katika gereza la Abu Salim
Kaburi la pamoja la mamia ya watu lagunduliwa mjini Tripoli, Libya.

Kaburi la pamoja linaloaminika kuwa na miili 1,270 limegunduliwa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli baraza la mpito la nchi hiyo limesema.

Mabaki hayo yanadhaniwa kuwa ya wafungwa waliouwawa na maafisa wa usalama mwaka wa 1996 katika gereza la Abu Salim.

Uasi dhidi ya Kanali Muammar Gaddafi ulianza kama maandamano kutaka wakili aliyewakilisha familia za wafungwa wa Abu Salim aachiliwe huru.

Uchimbuaji wa kaburi hilo la pamoja unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Baraza la mpito la kitaifa (NTC) liligundua kaburi hilo la pamoja- jangwa lililotawanyika sehemu za mifupa katika uwanja wa gereza la Abu Salim- baada ya kuwahoji walinzi wa gereza hilo waliofanya kazi wakati wafungwa hao waliuwawa baada ya kuadamana dhidi ya hali yao ya maisha.

Baadhi ya sehemu za mifupa na nguo zilizochanika tayari zimepatikana.


'makombora na risasi'


Baadhi ya familia walizuru eneo hilo, miongoni mwao akiwa Sami Assadi, ambaye alipoteza kaka wawili katika tukio hilo.

Alielezwa kaka zake walikufa kutokana na sababu za kawaida miaka mitano iliyopita. Alieleza BBC alivyojihisi alipofika mahali ambapo kaka zake huenda walizikwa.

''Nina hisia tofauti kwa hakika. Sote tulikuwa na furaha kwa sababu mageuzi haya yamefanikiwa lakini, wakati ninaposimama hapa nawakumbuka kaka zangu na marafiki wangu wengi sana ambao wameuwawa, na sababu hasa, ni kwamba hawakumpenda Muammar Gaddafi.''

Mwandishi wa BBC Jonathan Head ambaye alifika katika eneo hilo anasema, hadi hivi majuzi ni habari chache sana ndizo zilijulikana kuhusu mauaji ya wafungwa hao.

Watu wachache walioshuhudia tukio hilo wamelezea kuwa wafungwa hao waliuwawa katika seli zao kwa makombora na kupigwa risasi baada ya kuandamana.

Maafisa katika serikali mpya wanasema watahitaji kufanya uchunguzi wa kisasa kusaidia kujua kilichofanyika katika eneo hilo.