Mfalme wa Saudia Arabia ameahidi kuwa wanawake, kwa mara ya kwanza, wataweza kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, miaka mine kutoka sasa.
Wanawake wa Saudi Arabia hivi sasa wanabaguliwa sana, pamoja na kukatazwa kuendesha gari.
Mfalme Abdullah bin Abdelaziz alisema wanawake sasa wataweza kupiga kura na piya kugombea viti, na aliongeza kusema kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya kushauriana na viongozi wa kidini.

Mfalme wa Saudia Arabia piya alisema kuwa wanawake watakuwa na haki ya kujiunga na Baraza la Shura..baraza la mashauriano linaloteuliwa na mfalme.

Norah Alajaji ni mawanafunzi kutoka Saudi Arabia, anayesoma katika chuo kikuu mjini London, na aliiambia BBC kuwa hatua ya mfalme imempa moyo:

"Mimi nina matumaini makubwa.

Pamekuwa na kebehi kuhusu wanawake wa Saudia Arabia; na watu wanafikiri hatua hii ni ndogo na imechelewa mno, lakini mimi nafikiri hata safari ndefu huanza kwa hatua moja.

Na hii ni hatua kubwa, ya kuwapa uwezo wanawake."