Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete kufungua Kongamano la DICOTA mjini Dulles .
Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo kutoka kwa Victor Kileo na Wawila Hirji kuhusu utalii nchini Tanzania kwenye maonesho kabla ya kuhutubia Kongamano la Watanzania Mjini Dulles, Virginia.

 Na Mindi Kasiga,Dulles, Virginia - Marekani
Watanzania waishio Marekani wamesifia jitihada za Rais Kikwete za kuwashirikisha katika maendeleo ya Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi.
Hayo yamesemwa leo kwenye kilele cha Kongamano la Tatu la Watanzania Waishio Ughaibuni mjini hapa ambapo Watanzania zaidi ya mia tano wamehudhuria pamoja na makampuni, mashirika ya umma na binafsi zaidi ya 15 kutoka Tanzania yamehudhuria Kongamano hilo .
Miongoni mwa mambo yaliyokonga nyoyo za washiriki ni hotuba ya Rais Kikwete akifafanua masuala ya uraia pacha na haki ya kupiga kura kwa Watanzania walioko nje ya nchi kuingizwa kwenye mjadala wa Katiba mpya utakaofanyika hivi karibuni.
Kabla ya hotuba ya Rais, Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard Membe naye alimwaga sifa kwa Rais Kikwete na kusema Rais ni kinara wa kwanza wa kupigania maslahi ya Watanzania waishio nje ya nchi kwani ametambua umuhimu wao na ameelekeza Wizara yake kulipa suala hili kipaumbele.
Rais Kikwete aliwasihi Watanzania wasirudi nyuma katika kujiletea maendeleo hata kama wako mbali na nyumbani. Aliwataka wanunue viwanja na wajenge nyumba Tanznia. Wakati wa kongamano, suala zima la utoaji na umilikishwaji wa ardhi na ujenzi wa makazi kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi liliwasilishwa na Bwana Patrick Rutabanzibwa, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Manejimenti Utumishi wa Umma alizungumzia fursa zitakazotolewa na ofisi yake kupitia mradi wa UNDP utakao wawezesha Wataalamu wa Kitanzania waishio nje kuajiriwa kwa mikataba maalum ya kufanya kazi na kujenga uwezo ndani ya nchi kwenye taaluma hizo.
Kwa upande wa fursa za ajira, Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stergomena Tax, alizungumzia upatikanaji wa ajira ndani ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashiriki.
Akizungumzia furaha yake, Rais wa DICOTA Dr. Ndaga Mwakabuta amesema, “tumeguswa na ujio wa Rais Kikwete na Mawaziri walioongozana naye na Makatibu Wakuu hapa Marekani. Tumeona jinsi Rais anavyojali mchango wetu, ana imani na sisi, ametushirikisha na kuelekeza wasaidizi wake na watendaji waungane na sisi kwenye suala zima la uraia wa nchi mbili, hii ni faraja kubwa kwetu,” alisema Dr. Mwakabuta kwa furaha.
Wengine walisema Kongamano hili limewabadilisha fikra zao kuhusu utendaji kazi wa Serikali, ambapo sasa wanaimani ya kupata mafanikio kutokana na jitihada zinazofanywa na serikali ili kuwasaidia kupeleka maendeleo yao nyumbani na hatimaye kuinua uchumi wa Nchi.
Washiriki wengine walisifu waandaaji wa Kongamano hilo kwa kuandaa mada mbalimbali ambazo zimewafungua macho na kufanya waanze kufikiria njia bora zaidi za kuwekeza nyumbani.
“Nimependa sana na hotuba ya Rais Kikwete na Waziri wake wa Mambo ya Nje Membe. Nimefurahi kuona serikali inajitoa kiasi hiki kutambua mchango wa Watanzania walio nje, na kuwapa fursa ya kupeleka mchango huo nyumbani, hivi jirani zetu wanafanya hivi? Tunapendekeza tuwe na mkutano huu kila mwaka ili wengine waige mfano wetu” alisema Victor Kileo, mmoja wa washiriki wa Kongamano hilo kutoka Maryland.
Kongamano la DICOTA (Baraza la Watanzania Waishio Ughaibuni Marekani) hufanyika kila mwaka kuanzia mwaka 2009 kwa kuwaleta pamoja Watanzania kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.
Kongamano la mwaka huu katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru limeandaliwa na DICOTA kwa kushirikina na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia ubalozi wake wa Washington DC, chini ya usimamizi wa Balozi Mwanaidi Maajar.(toka Michuzi).