MASUALA ya uraia wa nchi mbili na haki ya kupiga kura kwa Watanzania walioko nje ya nchi yataingizwa kwenye rasimu ya mjadala wa Katiba mpya utakaofanyika hivi karibuni.

Rais Jakaya Kikwete amewaambia hayo Watanzania wanaoishi hapa wakati wa ufunguzi wa kongamano kubwa la Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi, linalofanyika jijini hapa.

"Suala la uraia wa nchi mbili ni jambo zuri, tunaliunga mkono pande zote, lakini ni suala la
kikatiba na hili litajadiliwa kwenye mjadala wa Katiba unaokuja pamoja na suala la Watanzania waishio nje kupiga kura,” Rais alisema. 

Ujumbe wa Kongamano hilo ni “Watanzania Ughaibuni Baada ya Miaka 50 ya Uhuru”.

Katika kongamano hilo Rais alisema Watanzania wana kila sababu ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru, kwani bado wamebaki kuwa wamoja kama nchi, jambo ambalo ni la kujivunia, kwa nchi yenye makabila mengi kubaki na amani si jambo dogo.

Kongamano la Watanzania pia linashirikisha baadhi ya taasisi za kiserikali, binafsi na biashara kutoka Tanzania na Marekani.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana tangu Uhuru, Rais alielezea hatua kubwa zilizofikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwamo elimu ambapo watoto wengi zaidi wako shuleni sasa
kulinganisha na kabla ya Uhuru.

Hivi leo, asilimia 97 ya watoto wako shule ya msingi ukilinganisha na asilimia 2 tu wakati wa
Uhuru, pamoja na hayo kuna shule za msingi 15,816 kulinganisha na shule 3,000 tu wakati Tanzania inapata Uhuru.

Leo hii Tanzania ina shule za sekondari 4,237 zinazoandikisha wanafunzi 1,638,699 kulinganishwa na shule 41 tu za sekondari zilizokuwa na wanafunzi 11,832.

Wakati wa Uhuru, Tanzania ilikuwa na wahitimu 13 tu wa Chuo Kikuu ilhali leo hii kuna wanazuoni 120,000 wanaosoma vyuo vikuu Tanzania, na wakati wa Uhuru kulikuwa na wahandisi wawili tu, leo hii wapo 11,4000 na pamoja na hayo, mafanikio haya ya Tanzania yametambuliwa duniani kote na kupata tuzo ya Malengo ya Milenia.

Rais alisisitiza kuwa miaka inayokuja, itakuwa ni muhimu katika kuboresha na kuongeza ubora wa elimu kwa kufundisha na kuajiri walimu zaidi, kuongeza vitabu na vifaa vya kufundishia,
zikiwamo maabara, nyumba za walimu na kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi na kuishi na hasa vijijini.

Mafanikio mengine ni kwenye afya, ambapo uwezo wa kupambana na maradhi umeongezeka, kuna zahanati, vituo na hospitali zaidi ambapo lengo la Serikali ni kuhakikisha kuna zahanati kila kilometa tano karibu na wananchi.

Tanzania pia imejijengea uwezo katika kupambana na maradhi kama vile Ukimwi, kifua kikuu, malaria, figo na moyo na sasa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka na vifo vya mama na mtoto vimepungua.

Katika miundombinu alisema kulikuwa na barabara zenye urefu wa kilometa 33,000 ambazo kati ya hizo kilometa 1,360 pekee ndizo zilikuwa za lami na leo hii kuna kilometa 86,672 ambapo kati ya hizo 6,500 ni za lami.

Rais aliwakumbusha Watanzania kutosahau nyumbani kwa kujenga nyumbani, kusaidia ndugu zao na kushiriki katika juhudi za kuleta vitega uchumi ikiwamo teknolojia na ujuzi mbalimbali ambao unahitajika nyumbani. Rais alikamilisha ziara yake ya kikazi Marekani na anatarajia kuondoka leo kurejea Tanzania.