Meneja wa Kampeni za Chadema katika uchaguzi mdogo wa Igunga, Tabora, Mwita Waitara akipanda gari kwenda kutoa maelezo katika kituo cha Polisi cha mjini Igunga kwa tuhuma za kutaka kumteka nyara Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Bulaya usiku wa kuamkia Septemba 24. (Na Mpigapicha Maalumu).

KAMPENI za uchaguzi wilayani hapa zimeingia sura mpya baada ya matusi majukwaani, vurugu za kumwagiana tindikali na sasa silaha za moto zimetumika.

Katika tukio la hivi karibuni, CCM inaituhumu Chadema kwa inachokieleza ni kuwafyatulia risasi wabunge wake.

Akizungumza katika ofisi za wilaya za CCM, Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Esther Bulaya, alidai kuwa juzi usiku wa kuamkia jana, akitoka Hoteli ya Silent Inn kwenda alikofikia, alifukuzwa na gari la Chadema likiwa na kada wa Chadema, Mwikwabe Mwita ambaye alikuwa akifyatua risasi angani.

Kwa mujibu wa madai hayo ya Ester, baada ya kuona Mwita akifyatua risasi angani, aliogopa kurudi kwenye hoteli alimofikia ya Peak Lodge na kuamua kukimbiza gari kwenda Singida.

"Baada ya kuona wanaendelea kunifukuza, nilimpigia simu Aishi (Hilary, Mbunge wa Sumbawanga Mjini), nikamwambia waje waniokoe nimetekwa naelekea upande wa Singida," alidai Bulaya.

Aliendelea kudai kwamba wakati anafukuzwa, gari lake lilipigwa mawe na risasi na kuharibiwa.

Ushahidi wa Aishi Aishi baada ya kupata simu hiyo, wakati akikaribia kufika Hoteli ya Peack Lodge, alidai kuwa alimwambia dereva wake ageuze gari kwenda kumfuata Bulaya na njiani waliona gari aina ya Toyota Double Cabin, likiwa na bendera ya Chadema likifukuza gari la Bulaya.

"Tukaamua kuwafuatilia lakini baada ya kuona gari langu likiwafuatilia, walikata kona na kuingia porini na kumwacha Esther na sisi tukawafuata na wakazunguka na kutokea katika hoteli yao ambapo geti la hoteli hiyo lilikuwa wazi, lile gari (Toyota Double Cabin) likaingia ndani moja kwa moja," alidai Aishi.

Wakiwa katika eneo hilo na kwa mujibu wa madai yao, walitoa taarifa Polisi, Aishi akadai kuwa
vijana wa Chadema walijitokeza na kulizingira gari lake na mmoja akalifyatulia risasi gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser na kuvunja vioo vya nyuma.

Chanzo cha ugomvi Chanzo cha ugomvi huo kwa mujibu wa Bulaya, ni mkutano wake wa kampeni za kumwombea kura mgombea wa CCM, Dk. Dalaly Kafumu katika kata ya Itumba.

Alidai akiwa njiani kwenda kwenye mkutano huo, Bulaya ambaye alikuwa na waandishi wawili wa habari katika gari lake, alidai waliona gari la Chadema likiwa limesimama katika nyumba ya mmoja wa viongozi wa CCM.

Aliendelea kudai kwamba alisimamisha gari lake na kwenda kwenye gari la Chadema na kuwakuta viongozi wa Chadema, Reuben Mtausigaye na Musa Hamis wakiwa na karatasi bandia ya kutambua wapigakura na daftari la wapigakura.

"Niliwafuata na kuhoji wametoa wapi nyaraka za Tume ya Uchaguzi (NEC), wakasema wamepewa na uongozi wa Chadema, lakini hawazitumii, niliwanyang'anya na kuzipeleka Polisi," alidai Bulaya.

Aliongeza kwamba Chadema wanatumia fomu hizo kununua shahada ili wananchi wasiende kupiga kura na kwa kuwa siri yao ilishagundulika, wakaanza kuwafuatilia.

Daftari la wapigakura
Naye Mratibu wa Kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba, alidai Chadema wana daftari la wapigakura lenye picha za wapiga kura na wanatembea nalo vijijini, kutisha wapigakura kuwa wasipoipigia kura Chadema, kompyuta itaonesha na watashughulikiwa.

Alidai kuwa wananchi wamekuwa na woga, kwa kuwa daftari hilo lina picha zao na wanazitumia kuwatisha.

Chadema yajibu tuhuma
Baada ya maelezo ya CCM, gazeti hili lilifika Polisi kupata uthibitisho, lakini kabla ya Polisi kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema na Mbunge wa Iramba Mashariki, Tundu Lissu, aliingia katika kituo hicho cha Polisi na baadaye akatoka nje kuzungumza na waandishi.

Kwa mujibu wa madai ya Lissu, Chadema ndio walivamiwa na vijana wa CCM katika hoteli yao wakiongozwa na Aishi na Bulaya, lakini vijana wa Chadema wakalidhibiti gari la Mbunge huyo wa Sumbawanga.

Kutokana na kudhibitiwa kwa gari lake, Lissu alidai mbunge huyo alifyatua risasi angani, lakini
hakufanikiwa kulichukua gari hilo mpaka Polisi walipofika na kulichukua.

Lissu alisema hali hiyo imewatisha na wakichanganya na kitendo cha mbunge mwingine wa CCM, Ismail Rage wa Tabora Mjini kupanda jukwaani na bastola kiunoni, wameandika barua kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuomba CCM na mgombea wake waondolewe katika kinyang'anyiro hicho cha uchaguzi.

Aliwalaumu polisi kwa kutowaweka ndani Aishi na Rage ambao alidai ni wahalifu, na badala yake wakawapekua Mwita na dereva wake na katika upekuzi huo hawakukutwa na kitu.

Lakini pia alikiri kwamba Chadema ina daftari la wapigakura wa nchi nzima na kuongeza kuwa vyama vyote vilipewa na NEC na wanalitumia kudhibiti wapigakura mamluki, lakini kwa kuwa CCM ni wazee hawajui kutumia kompyuta, ndiyo maana wanalalamika.

Polisi na uchunguzi
Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Polisi Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu, baadaye alisema wanafanya upelelezi wa suala hilo.

Alifafanua kuwa tayari watu wapatao 10, wakiwamo Bulaya, Aishi na Mwita, waliitwa na kuandikisha maelezo na pia waliokota maganda matatu ya risasi za bastola yenye mtutu wa milimita tisa.

Mngulu alisema pia wanashikilia magari ya Bulaya na Aishi na kufafanua kuwa hana hakika kama kuna lililopigwa risasi, lakini la Bulaya, aina ya Prado limetobolewa kioo cha nyuma matundu matatu kwa alichokisema ni mawe na la Aishi, huenda ndilo lilipigwa risasi kwa kuwa vioo vyake vimesambaratika kabisa.

CUF wafurahia
Wakati hali ikiendelea, gari la matangazo la CUF lilipita njiani likiwataka wananchi wa Igunga kuchagua mgombea wake, Leopold Mahona, kwa madai kuwa Chadema na CCM wameshindwa kutunza amani ya Igunga na sasa wanarushiana risasi.

Source-Habari Leo.