Niger inasema kuwa Saadi Gaddafi, mmoja wa watoto wa kiume wa kiongozi wa Libya aliyeondolewa madarakani Muammar Gaddafi, amewasili katika mji mkuu, Niamey.

Saadi Gaddafi alivuka mpaka kutoka Libya mwishoni mwa juma na akapewa hifadhi, maafisa wa Niger walithibitisha.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema "yuko chini ya kifungo cha nyumbani", ingawa Niger haijathibitisha hilo.

Gaddafi mwenyewe hajulikani yuko wapi. Amesema kuwa yuko tayari kufariki dunia akiwa Libya kuliko kutoka nje ya nchi.

Inasemekana Saadi Gaddafi alisafirishwa kwa ndege ya kijeshi hadi Niamey kutoka kaskazini mwa Niger,mji wa Agadez.

Chanzo kimoja cha habari mjini Niger kilitoa taarifa kwa shirika la habari la AFP kusema kuwa Saadi "yuko salama" chini ya maafisa wa usalama wa Niger mjini Niamey.

Chanzo hicho kilisema kuwa awali alikuwa anaishi katika nyumba ya gavana wa Agadez.

Kufikia sasa washirika 32 wa karibu wa Gaddafi - wakiwemo majenerali watatu wa kijeshi - wameingia Niger mwezi huu.