Kashfa nzito imeikumba Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam baada ya baadhi ya madaktari kulalamikiwa kumfanyia kitendo cha unyama mama mmoja mjamzito kwa kumuacha mtoto mfu tumboni kwa siku tatu.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Agosti 28, mwaka huu mara baada ya mwanamke huo Leah Joseph (33) mkazi wa Chanika kufikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kuonyesha dalili ya mimba yake kuharibika.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, mume wa mwanamke huyo Joseph Mrangu (42), alisema mkewe ambaye alikuwa na mimba ya miezi mitano alifikishwa hospitalini majira ya saa tatu asubuhi siku ya tukio baada ya kulalamika kuumwa na tumbo pamoja na kuonyesha dalili ya mimba kuharibika.
Alisema baada ya kufika hapo daktari aliwaeleza apelekwe wodi namba 10 ambapo alipatiwa kitanda na huduma ya kusafishwa kwa gharama kutokana na kubainika mimba yake iliharibika.
Mrangu alisema katika gharama hizo alitoa Sh 38, 000 ikiwa ni gharama za kusafisha kizazi usafishaji Sh. 24,000, kitanda Sh. 4,000 na vifaa vya huduma Sh.10,000. "Nilitoa pesa zote kama walivyotaka madaktari, baada ya muda walimpeleka mke wangu katika chumba maalum cha kumsafishia," alisema Mrangu.
Alieleza mara baada ya kazi ya kusafishwa kumalizika alipewa cheti kumruhusu kikionyesha hakuna kiumbe ndani ya tumbo la mama na kurejea nyumbani.
Waliporudi waliendelea kumpatia dawa za kutuliza maumivu kwa siku mbili na ilipofika siku ya tatu alishangazwa kuona hali ya mkewe imebadilika na kuwa
mbaya.
Akiwa anatafuta ufumbuzi wa jambo hilo, mkewe alikwenda chooni kujisaidia, lakini akiwa huko alisikia sauti ya mkewe ikimuita na ndipo alishtuka kuona kitu kinatoka sehemu zake za uzazi, ndipo alipomuita jirani yao aje kuwasaidia.
Kutokana na hali hiyo waliamua kumpeleka haraka katika zahanati ya Buyuni ambayo ipo jirani na eneo wanaloishi na baada ya uchunguzi ilibainika mkewe alikuwa bado ana mtoto tumboni kwani madaktari waliomsafisha awali hawakumtoa mtoto huyo.
"Nilishangazwa na maelezo ya wale madaktari kwani cheti cha hospitali ya Amana kinaonyesha hakuna mtoto," alisema Mrangu.
Aliendelea kusema "Sikuamini kauli ile hadi pale madaktari walipofanikiwa kumtoa mtoto ambaye alikamilika viungo vyote,"
Alisema Kitendo hicho cha madaktari kutoa ripoti ya uongo kimemsikitisha na kinaonyesha ni jinsi gani baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo wasivyothamini maisha ya watu na badala yake wanafanya kazi kwa kulipua.
Marangu alisema anawashukuru madaktari wa zahanati ya Buyuni kwa kuokoa maisha ya mkewe kwa kufanikiwa kumuondoa mtoto huyo tumboni.
Naye jirani aliyeshuhudia tukio hilo, Mariam Juma (30), alisema haimuingii akilini kitendo kilichofanywa na madaktari wa Amana kwani ujauzito wa Leah ulikuwa wa miezi mitano na kama kiumbe kinakuwa kimekamilika kitu ambacho ni rahisi kuona wakati kikitoka.
"Itakuwaje wale wa Buyuni waone bado kulikuwa na mtoto tumboni na ile Hospitali kubwa wasione, mambo haya wanayofanya yanahatarisha maisha kwani kuishi na kiumbe mfu kwa siku tatu ni hatari," alisema Mariam.
Aidha, alisema hata madaktari walipowashauri warudi tena Amana kwa ajili ya kumpatia Leah matibabu zaidi iliwapa wakati mgumu kuafiki maamuzi hayo lakini kutokana na madaktari hao kusisitiza na kupatiwa gari la wagonjwa iliwabidi kukubali.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Asha Mahita alipopigiwa simu kuelezea tukio hilo, alisema bado suala hilo halijamfikia na kuahidi kuwasiliana na Mganga wa Hospitali hiyo ili kupata ufafanuzi zaidi.