Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa wananchi aliyoitoa juzi, Rais Kikwete alisema Serikali imejiandaa vya kutosha kutimiza ipasavyo wajibu wake wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa Igunga katika kipindi hiki cha uchaguzi na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila wasiwasi wowote.
“Hatukubali siku ya kupiga kura iwe ni siku ya watu kujifungia ndani au kuogopa kutoka nje. Nawahakikishia hilo halitatokea huko Igunga. Na wanaodhani kuwa tunatania wathubutu, watadhibitiwa ipasavyo,” alisisitiza.
Aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kumchagua mtu wanayemtaka kuwa Mbunge wao kwa kupiga kura. “Haitakuwa sawa hata kidogo kama ndugu zetu wa Igunga wataacha kutimiza wajibu wao huo wa msingi kama raia.”
“Nawasihi, wananchi wa Igunga kuendelea kudumisha amani, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa. Nawaomba msikubali wanasiasa wawageuze chambo cha kuendeleza maslahi yao binafsi ya kisiasa na tamaa zao za madaraka zilizovuka mipaka,” alisema.
Alisisitiza kuwa amani ya nchi ni tunu adhimu ya taifa iliyorithiwa kutoka kwa waasisi wa taifa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume.
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeshawahakikishia wapiga kura wa Igunga kwamba maandalizi yote yamekamilika na shughuli za uchaguzi zitakwenda kama inavyotarajiwa. “Wamesema vifaa vyote tayari vimesambazwa katika kata zote, wasimamizi wa vituo na mawakala wa vyama wamekamilika. Kwa jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyojipanga, ninayo imani kuwa mchakato mzima wa uchaguzi utakwenda vizuri”, alisistiza.
AJALI MELI MV SPICE ISLANDER
Akizungumzia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander iliyoua mamia ya watu Septemba 10, mwaka huu, Rais Kikwete alisema mara baada ya taarifa ya ajali hiyo hatua zilichukuliwa za kuokoa watu, meli na mali iliyokuwamo. “Bahati nzuri ndugu zetu 619 waliweza kuokolewa wakiwa hai na sasa wanaendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa na kujiletea maendeleo yao. Maiti 203 waliweza kupatikana na kuzikwa kwa heshima. Maiti 197 walipatikana eneo la tukio, tano walipatikana Kenya na mmoja Tanga. Maiti waliopatikana eneo la tukio walizikwa Unguja na wale waliopatikana Kenya na Tanga walizikwa huko huko”, alisema.
Hata hivyo alisema hakuna uhakika kama wapo watu waliozama pamoja na meli hiyo au hapana. Bahati mbaya idadi kamili ya watu waliokuwamo katika meli hiyo haijulikani kwa uhakika. Orodha rasmi ya wenye meli inaonyesha idadi ya watu waliokuwemo kwenye meli wakati inaondoka bandari ya Malindi, Zanzibar kuwa pungufu kuliko idadi ya watu waliookolewa na maiti waliopatikana. Kwa sababu hiyo, huenda wapo watu waliozama na meli na kushindwa kutoka, alisema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amekwishaunda Tume ya Uchunguzi ambayo baada ya kumaliza kazi yake ndipo undani kuhusu ajali hiyo utapoweza kujulikana. Tume hiyo imekwishaanza kazi na kama kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, baada ya mwezi mmoja wataimaliza kazi hiyo.
Alivipongeza vyombo vya usalama na wale wote walioshiriki kuokoa maisha ya watu waliozama na kuwaopoa maiti.
SAFARI ZAKE MAREKANI
Kuhusu safari yake ya Marekani Septemba 16 na 23 ya kuhudhuria Kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na shughuli zake, alisema alihudhuria pia mikutano mingine kama Open Government, ulioitishwa na Rais Barrack Obama wa Marekani, Mkutano wa Umoja wa Marais wa Afrika wa kupambana na malaria, Mkutano wa Tatu wa Watanzania Waishio Marekani (DICOTA 3) na mkutano kuhusu Wanawake na Lishe ulioandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mama Hilary Clinton.
Aidha, Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Stephem Harper wa Canada waliwasilisha taarifa ya Tume ya Afya ya Mama na Mtoto aliyoiunda Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambayo walikuwa wenyeviti wenza. “Nafurahi kwamba taarifa yetu imepokelewa vizuri na kuelezwa kuwa itakuwa msingi mzuri wa kutatua matatizo ya vifo vya kina mama na watoto duniani.”
Alisema, katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alieleza jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa katika miaka 50 ya uanachama ambayo pia ndiyo miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
MARADHI YASIYOAMBUKIZA
Alisema katika kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kulifanyika mkutano maalum kuhusu maradhi yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo, shinikizo la damu, figo na saratani. Kwa muda mrefu dunia imejishughulisha na maradhi yanayoambukiza kwa vile yamekuwa yanaua watu wengi, kwa mfano malaria, Ukimwi na kifua kikuu lakini, ni ukweli ulio wazi kwamba siku hizi maradhi yasiyoambukiza nayo yamekuwa chanzo kikubwa cha watu wengi kupoteza maisha.
Kwa kutambua ukweli huo, imeonekana upo umuhimu kwa Umoja wa Mataifa kujihusisha kwa karibu katika kupambana na maradhi hayo kama inavyofanya kwa maradhi ya kuambukiza. “Baada ya mkutano maalum wa tarehe 19 – 20 Septemba, 2011, tutegemee mabadiliko makubwa yenye tija na manufaa kwa wanadamu katika kukabiliana na maradhi haya.
Rais Kikwete aliongeza kuwa Tanzania imepata heshima nyingine kubwa kufuatia uamuzi wa Rais Barack Obama wa Marekani wa kuijumuisha katika kundi la nchi 46 duniani zitakazoshiriki katika mpango mpya unaoitwa Open Government Partnership. Mpango ulianza na nchi nane, Afrika ya Kusini ikiwa ndiyo nchi pekee ya Afrika. Sasa zimeongezeka nchi nne za Tanzania, Kenya, Ghana na Liberia na kufanya nchi za Afrika kuwa tano kati ya hizo 46 duniani.
Sifa kubwa ya nchi kujumuishwa katika mpango huo ni Serikali kuwekeza katika maendeleo ya watu wake na kuongoza kwa misingi ya kidemokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
TUZO
Akizungumzia tuzo alizopata, Rais Kikwete alisema
“Juhudi tuzifanyazo za kupambana na changamoto mbalimbali ili kujiletea maendeleo zimeonekana na kutambuliwa duniani. Bila ya kutarajia nchi yetu imepewa tuzo tatu za heshima kimataifa kutokana na mafanikio tunayoyapata katika nyanja mbalimbali. Tuzo hizo za kimataifa nilizopewa mimi ni za nchi yetu na watu wake.”
Mkutano na Watanzania wa Marekani
Kuhusu mkutano wake na Watanzani wanaoishi Marekani, Rais Kikwete aliwaambia aliwaomba wawe raia wema katika nchi ya watu na kuwasihi wajiepushe kufanya vitendo vya uhalifu kama vile wizi, ujambazi, kutumia au kufanya biashara ya dawa za kulevya na ubakaji.
Aidha, aliwataka wasisahau nyumbani kwao. Wametoka huku nyumbani kwenda nje kuchuma ili wajiletee maendeleo. Wakumbuke kujenga nyumba nzuri kwao ili wawe na mahali pazuri pa kufikia. Wakati mwingine kukosa mahali pazuri pa kufikia kunawafanya wasije nyumbani au wakija waishie mjini kwa sababu nyumbani kwao hakuwafai kwa viwango vyao.
Aliwaomba wawe na umoja wao ili uwe ndicho chombo cha kuwaunganisha na kuratibu shughuli zao. Pia kiwe ni chombo cha wao kusaidiana wawapo na shida kama vile misiba. “Nafurahi kwamba wamekwishaunda chombo hicho yaani DICOTA. Bahati nzuri kwa upande wa kusaidiana, viongozi wa DICOTA wameshazungumza na NSSF ambao wameanzisha aina fulani ya bima ya afya ambayo watu watachangia na mtu akipoteza maisha, mwili wake utasafirishwa kwa gharama ya NSSF. Aidha, huku nyumbani kwao nako, ndugu zake atakaowachagua watapata matibabu kwa gharama ya NSSF.
URAIA WA NCHI MBILI
Alisema moja ya kilio cha siku nyingi cha Watanzania waishio nchi za nje ni kupata fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili, yaani wa Tanzania na wa ile nchi ya nje anayoishi. “Niliwaeleza kuwa tumekisikia kilio chao na tunaelewa kuwa zipo nchi nyingi duniani zinao utaratibu huo.
Bahati mbaya sisi hatuna utaratibu huo, lakini tunafikiria suala hilo liwe miongoni mwa mambo ambayo yatazungumzwa katika mjadala wa Katiba mpya ili wananchi waamue. Kuhusu fursa ya kupiga kura nje ya nchi ni suala ambalo tutalizungumza kupitia taasisi husika.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments