Shughuli za misaada karibu na mpaka kati ya Kenya na Somalia zimepunguzwa kufuatia kutekwa nyara kwa wafanyakazi wawili wanawake wa utoaji misaada, msemaji wa Umoja wa Mataifa ameiambia BBC.
Shughuli zote za kusaidia kuokoa maisha kwa sasa zimesitishwa, lakini usambazaji wa maji, chakula na huduma za afya zinaendelea, amesema Emmanuel Nyabera wa UNHCR.
Karibu watu nusu milioni wamekimbia ukame na mapigano nchini Somalia na wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Daadab.

Polisi wa Kenya wamesema wanaamini wafanyakazi wawili wa shirika la MSF kutoka Uhispania waliotekwa wanashikiliwa nchini Somalia.



Bw Nyabera amesema kusitishwa huko kwa shughuli kutakuwa kwa siku kadhaa wakati hali ya usalama ikifanyiwa marekebisho katika eneo hilo.

Mwandishi wa BBC Bashkash Jugsodaay aliyepo Daadab amesema shule zimefungwa na MSF imeondoa baadhi ya wafanyakazi wake katika eneo hilo kufuatia utekaji nyara.

Kuna hali ya wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi wa utoaji misaada na katika kambi ya wakimbizi ya Daadab, ambayo kwa sasa imekuwa kama jiji la tatu kwa ukubwa nchini Kenya kutokana na idadi ya watu, ambao wamekimbia ukame mbaya kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka 60.

Somalia ndio imeathirika zaidi, huku baadhi ya maeneo yakitangawa kuwa ni maeneo yenye njaa kali, na maelfu ya watu wanakimbia makazi yao kutafuta msaada.