Polisi katika kizuizi cha Nkende Magena kilichopo barabara kuu ya Tarime - Sirari mpakani, wameyakamata magari mawili yakiwa yamesheheni mifuko 400 ya sukari ya uzito wa kilo 50 kila mmoja ikisafirishwa kwenda nchini Kenya bila kibali.
Magari yaliyokamatwa ni yenye namba za usajili T 577 BAQ lori aina ya Scania na gari la abiria aina ya Hiace yenye namba za usajili T 803 AWR.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele na Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, SSP Mayambuga, wamethibitisha kukamatwa kwa magari hayo yakiwa na shehena ya sukari.
Lori hilo aina ya Scania T577 BAQ, ni mali ya Salum Said, mkazi wa mkoani Shinyanga ambapo alikamatwa nalo Mwalimu wa Shule ya Msingi Saba Saba, Lucas Wambura, likiwa na mifuko 350 kila mmoja ukiwa na uzito wa kilo 50 za sukari na Hiace T 803 AWR alikamatwa nalo Mussa Mabere, mkazi wa Sirari likiwa na mifuko 50 ya sukari.
Henjewele amewaagiza askari wa Usalama Barabarani katika wilaya hiyo ya Tarime kuanzia vituo vya Kirumi, Komaswa, Gamasara, Nkende na Sirari, kuhakikisha kwamba wazuia magari ya mizigo kutoka Mwanza kuanzia saa 12:00 jioni kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayopitishwa kwa magendo usiku.
Alisema wapo mawakala bandia zaidi ya 80 baadhi yao wakitokea nchini Kenya ambao hujihusisha kusafirisha sukari, mahindi na mchele usiku kwenda nchini Kenya na hivyo kuihujumu nchi.
Henjewele aliagiza sukari yote iliyokamatwa kupelekwa katika uwanja wa mpira Saba Saba mjini Tarime na kuuziwa wananchi kwa bei elekezi ya serikali ambapo mfuko mmoja wa kilo 50 utauzwa kwa Sh. 107,000.
Aidha, aliwaonya mawakala hao bandia kuwa serikali itawachukulia hatua kali za kisheria za kufanya biashara ya magendo na kuhujumu uchumi wa nchi.
Bei ya sukari katika Wilaya za Tarime na Rorya imepanda kutoka Sh. 1,700 hadi Sh. 4,000 kwa kilo moja hali inayosababisha familia nyingi zishindwe kumudu kuinunua.
Wakati huo huo, dereva wa lori lililokamatwa likiwasafirisha Waethiopia 73 kuingia nchini kupitia mpaka wa Kijiji cha Kogaja wilayani Rorya, Ally Mbula, amehukumiwa kulipa faini ya Shilingi milioni mbli ama kwenda jela miaka mitatu baada ya kukiri kosa la kuwasafirisha raia wa kigeni kuingia nchini bila vibali. Aidha, raia hao wa kigeni wameamriwa kulipa faini ya Sh. 100,000 kila mmoja ama kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja.
Hata hivyo, dereva na Wahabeshi hao walilipa faini hiyo.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo, Yusto Ruboroga.
0 Comments