Kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikipita mbele ya Jukwaa Kuu na kutoa heshima kwa mgeni wa rasmi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (hayupo pichani) kwenye kilele cha sherehe za kuadhimisha Miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Picha na Ramadhan Othman, Ikulu).

DALILI NZURI ZA MSHIKAMANO DHADHIHIRIKA JANA,HAKUNA UPEMBA WALA UUNGUJA WOTE WASHEHEREKEA PAMOJA.

SHEREHE za miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan jana zilifana huku zikionesha kurejea kwa mshikamano mkubwa wa wananchi wa Unguja na Pemba,
ambao sasa wameweka pembeni itikadi za vyama na kuweka utaifa mbele.

Sherehe hizo zilifanyika huku Wazanzibari wakiunganishwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotokana na maridhiano ya kisiasa ambayo lengo lake ni kuondosha siasa za chuki na uhasama.

Mbwembwe za viongozi wa kitaifa wakati wakiingia katika Uwanja wa Amaan pamoja na
gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama, ni miongoni mwa matukio muhimu ambayo yalifanikisha na kupamba sherehe hizo.

Wananchi walishangilia viongozi wao wa kitaifa akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed
Shein, ambaye aliingia uwanjani akisindikizwa na pikipiki za askari wa Polisi zaidi ya 10.

Lakini aliyevutia zaidi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jakaya Kikwete, ambaye alipokewa kwa kupigwa Wimbo wa Taifa.
“Ni sherehe ambazo zinatakiwa kuendelea kusherehekewa kila mwaka kwa lengo la vizazi vijavyo kujua na kutambua tunatoka wapi na tunakwenda wapi,” alisema mmoja wa waasisi wa
Mapinduzi, Hassan Nassoro Moyo, wakati akizungumza na gazeti hili.

Moyo alisema kauli hiyo kufuatia baadhi ya watu wakipinga kufanyika kwa sherehe hizo
ambazo hutumia fedha nyingi, huku wananchi wakihitaji huduma muhimu ambazo hazipatikani.



Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya miaka 48 zimetumia jumla ya Sh milioni 700 kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud.

Aidha, wananchi walijitokeza mapema na kuingia Amaan saa moja asubuhi bila kujali ukali wa
jua.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wananchi wengi kutoka Pemba ambao walifika hapa kwa usafiri wa boti na meli.

“Sherehe zimefana kweli kweli huku zikionesha mshikamano wa wananchi wa Unguja na
Pemba, ambao sasa wameungana na kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa,” alisema Juma Jongo.

Akihutubia umati uliojumuika Amaan, Dk. Shein alisema malengo ya Mapinduzi ya mwaka
1964 yataendelea kutekelezwa ikiwamo kuwapatia wananchi huduma muhimu na maendeleo bila ubaguzi.

Alisema malengo hayo ni muhimu kutekelezwa na kusimamiwa kikamilifu, kwani ndiyo yaliyofanya wananchi wa Zanzibar kufanya mapinduzi na kumwondoa mkoloni.Aliongeza kuwa huduma za maji safi na salama, elimu kwa watoto wote wenye uwezo wa
kwenda shule na huduma za afya na kutunza wazee wasiojiweza, zitaendelea kutolewa.

Alisisitiza umoja na mshikamano wa wananchi wa Unguja na Pemba akisema ndiyo siri ya
mafanikio yote ya utulivu wa kisiasa, huku akisisitiza pia kuimarishwa kwa Muungano na kupatiwa ufumbuzi wa kero zilizopo kupitia Kamati ya Pamoja chini ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilali.

Akifafanua kuhusu hali ya uchumi na changamoto zinazoikabili Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Dk. Shein alisema hali ya uchumi ni ngumu kutokana na mfumuko wa bei za vyakula
na kuongezeka kwa vitendo vya uharamia.

Alisema kasi ya ukuaji wa uchumi imefikia asilimia 6.5 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.7
mwaka 2009 na ukuaji mdogo wa sekta ya viwanda na huduma ambapo mwaka 2010 ukuaji wa
huduma ulifikia asilimia 8.7.

Kwa upande wa mfumuko wa bei alisema ni tatizo kubwa na umekua kwa asilimia 6.6 kwa
Januari mwaka juzi na mwaka jana hadi asilimia 18.7.

Hata hivyo, alisema SMZ imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na matatizo hayo ikiwamo
kupunguza ushuru kwa bidhaa muhimu za vyakula ukiwamo mchele na unga wa ngano.

Alisema SMZ inaendelea kutekeleza sera na mapinduzi ya kilimo katika uzalishaji wa chakula
na kupunguza kutegemea kuagiza bidhaa muhimu ukiwamo mchele kutoka nje.

Kuhusu mafanikio, aliitaja sekta ya miundombinu ya barabara, kwamba imeleta mapinduzi
makubwa ya uchumi na sasa barabara nyingi za vijijini zipo katika hali nzuri kwa kiwango cha
lami.

Alisema taasisi za ukusanyaji wa kodi ikiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA) na Bodi ya Mapato
(ZRB) zimefanya vizuri na kuvuka lengo la kukusanya mapato kwa asilimia 10 kutoka Sh bilioni
171.68 hadi Sh bilioni 181.48.

Mapema aliwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika
mchakato wa marekebisho ya Katiba wakati ukifika.