Gladness Mallya na Rhobi Chacha
‘BURIANI Mzee Kipara!’ Ndiyo maneno yanayoweza kumtoka binadamu yeyote aliyeshuhudia maisha ya mateso ya mzee huyo kabla ya kukutwa na mauti, aya zifuatazo zinaweza kukutoa machozi.
Fundi Said maarufu kwa jina la Mzee Kipara, alikuwa msanii mkongwe katika tasnia ya uigizaji Bongo, aliyetumia sehemu kubwa ya maisha yake katika sanaa ambaye juzi (Jumatano), Januari 11, mwaka huu, saa 2:00 asubuhi, Mungu alimchukua baada ya maumivu ya muda mrefu.
Mzee Kipara aliyeanza kusikika kwenye maigizo ya Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD, sasa TBC Taifa), alifariki dunia katika nyumba aliyokuwa amepangishiwa na Kundi la Sanaa la Kaole iliyopo Kigogo Mbuyuni, Dar es Salaam.
SIKU MOJA KABLA YA KIFO
Siku moja kabla ya kifo (Jumanne), Ijumaa lilifika nyumbani hapo kumjulia hali, ndipo lilishuhudia mzee huyo aliyekuwa na miaka 89, akiwa amekata kauli.
MATESO MAKUBWA KULIKO JINA LAKE
Mzee Kipara ambaye siku za hivi karibuni alikuwa akiishi maisha ya mateso makubwa kuliko jina lake kufuatia kutelekezwa na wahusika kulinganisha na kazi aliyoifanya ya kuelimisha na kuburudisha jamii, alikuwa hawezi kugeuka kitandani zaidi ya kukoroma.
HALI YAENDELEA KUWA MBAYA HADI GIZA LINAINGIA
Pia Ijumaa lilishuhudia daktari akimpatia matibabu ikiwa ni pamoja na kumtundikia ‘dripu’ ya kumuongezea maji mwilini, lakini mambo yalizidi kuwa mabaya hadi giza lilipoingia.



MAHOJIANO NA ALIYEKUWA AKIMHUDUMIA
Kabla ya kuondoka nyumbani hapo, Ijumaa lilifanya mahojiano na mwigizaji aliyekuwa akimhudumia aitwaye Mariam Athuman ‘Kalunde’;
Ijumaa: Hii hali ya kukata kauli ya Mzee Kipara ilianza lini?
Kalunde: Katika siku za hivi karibuni hali ilikuwa ya kuridhisha sana, ila miguu ndiyo ilikuwa bado inamsumbua.
Ijumaa: Sasa amefikiaje hali hii ya kutozungumza na kukoroma tu?
Kalunde: Kusema kweli hata mimi sijui shetani gani ameingilia kati.

DAKTARI ALISEMAJE?
Kwa mujibu wa daktari aliyekuwa akimpatia matibabu Mzee Kipara siku hiyo(aliomba asitajwe), haikujulikana mara moja ni ugonjwa gani uliokuwa ukimsumbua kwani wataalamu hawakupata historia yake kwa kina.

TAARIFA MBAYA
Jumatano saa 2:45 asubuhi, Ijumaa lilipokea simu kutoka ‘sosi’ ambaye ni jirani wa Mzee Kipara ambapo mazungumzo yalikuwa hivi;
Sosi: Najua hii ni namba ya Ijumaa, hapa nina taarifa mbaya.Ijumaa: Una taarifa gani mbaya?
Sosi: Jamani Ijumaa Mzee Kipara amefariki dunia.
NCHI NZIMA YAMWAGA MACHOZI
Kuanzia hapo, chumba chetu cha habari kiliendelea kupokea simu kutoka kona mbalimbali nchini zikimlilia Mzee Kipara.
Baada ya taarifa hiyo ya kuhuzunisha, Ijumaa lilifika katika nyumba aliyokuwa akiishi mzee huyo na kukuta watu wakiwa na simanzi huku wengine wakiangua vilio.

KILICHOMUUA CHAJULIKANA
Mara kadhaa Mzee Kipara alilalamika kusumbuliwa na miguu ambayo ilikuwa ikivimba ambapo kwa mujibu wa daktari wa Ijumaa, kilichomuua ni high blood pressure inayosababisha moyo kupanuka na kushindwa kufanya kazi, kitaalamu huitwa Congestive Cardiac Failure (CCF).
Hali hiyo husababisha moyo kushindwa kusukuma maji kutoka chini kwenda juu, hivyo miguu kuvimba na ugonjwa huo kitaalamu huitwa Oedema.

HISTORIA YAKE KATIKA SANAA
Mzee Kipara alianza sanaa mwaka 1964 kwa kufanya kazi za mitaani, mwaka 1966 alichukuliwa na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) sasa TBC Taifa.
Akiwa na kituo hicho, aliigiza michezo mingi na nafasi zake kubwa zilikuwa zile zenye kuonesha utemi.
Mwaka 1999, akiwa na wasanii wenzake, akina Zena Dilip, Rasia Makuka, marehemu Mzee Pwagu na Mama Haambiliki, walijiunga na Kundi la Sanaa la Kaole ambalo lilikuwa likirusha maigizo yake katika Runinga ya ITV.
ASILI YAKE
Mzee Kipara aliishi sehemu nyingi katika Jiji la Dar kama vile, Gerezani, Ilala na Kigamboni, lakini asili yake ni Mkoa wa Tabora.

FAMILIA
Akizungumza na Ijumaa kuhusu ilipo familia yake siku chache kabla ya kukutwa na umauti, Mzee Kipara alisema:
“Nakumbuka nilifiwa na mwanangu Said Fundi niliyezaa na mke wangu wa pili, Zena mwaka 1980, ilikuwa ni baada ya kuachana na mke wa kwanza aliyeitwa Msimu niliyemuoa mwaka 1970.

AMEWAFUATA RAFIKI ZAKE PWAGU NA PWAGUZI
Mzee Kipara amewafuata rafiki zake aliokuwa akiigiza nao waliotangulia mbele ya haki, Rajab Hatia ‘Mzee Pwagu’ na Ali Keto ‘Pwaguzi’.

WASANII VILIO
Wasanii mbalimbali wa Kaole, wakiongozwa na Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, Rajab Ally ‘Mzee Faki’, Ramadhani Mwishehe ‘Mashaka’ na wengine wengi walifika nyumbani hapo huku vilio vikisikika kila kona.
Mzee Kipara alitarajiwa kuzikwa jana katika makaburi ya Kigogo jijini Dar es Salaam.