Wananchi wakishuka kutoka kwenye kivuko cha mv Magogoni jijini Dar es Salaam. Serikali Januari mosi ilipandisha nauli katika kivuko hicho kutoka Sh 100 hadi 200/-. Kwa muda wa miaka 14 iliyopita kivuko cha Kigamboni kimekuwa kikitoza nauli ya Sh 100 kwa mtu mzima. (Picha na Mohamed Mambo).
MAGUFULI ATAKIWA KUOMBA RADHI WANANCHI WAKE KWA KAULI YAKE
WABUNGE wa Mkoa wa Dar es Salaam wamemjia juu Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwa
kupandisha nauli ya kivuko cha mv Magogoni na kumtaka awaombe radhi wakazi wa Kigamboni kwa kauli aliyoitoa kwao.
Wakizungumza jana katika ofisi ya Mbunge wa Ilala iliyoko Boma, Dar es Salaam, wabunge hao walisema kitendo cha Magufuli kutangaza ongezeko la nauli ya kivuko hicho kwa asilimia 100
bila kushirikisha wananchi, hakina tofauti na udikteta.
Katibu wa Umoja wa Wabunge wa Dar es Salaam, John Mnyika wa Ubungo – Chadema, alisema uamuzi wa wizara hiyo kupandisha nauli hiyo, umepokewa kwa mshituko na wabunge na wananchi wa Dar es Salaam na hivyo waliitaka Serikali kutathimini upya uamuzi huo.
Alisema jambo lolote linalotakiwa kufanywa na Serikali wananchi wanapaswa kufahamishwa, na si Wizara ikurupuke na kupandisha nauli bila wananchi kutaarifiwa, suala alilodai kuwa ni ubabe kufikia uamuzi.
“Anachokifanya Magufuli ni ukiukaji wa misingi ya utawala bora, yeye akiwa kiongozi wa wizara kwanza alipaswa kushirikisha wananchi katika kutoa uamuzi wa jambo hilo ili nao watoe mchango wao wa mawazo,” alisema Mnyika. Alisema hata kama kiongozi huyo anajitetea kuwa wizara ilitoa tangazo katika Gazeti la Serikali, kuhusu kupandishwa kwa nauli hiyo, wananchi wengi hawapati fursa ya kuliona wala kulisoma gazeti hilo, jambo alilosema kuwa lisingeweza kufikia wote.
Alisema kilichopaswa kufanywa na wizara, ni kuangalia kwanza namna ambavyo wangeweza kudhibiti mapato kutokana na ufujaji uliopo katika kivuko hicho, badala ya kukimbilia kupandisha bei.
Mnyika alikwenda mbali na kudai kuwa kauli ya Magufuli kuwataka wakazi wa Kigamboni
kupiga mbizi ili kuvuka eneo la bahari, kuwa ni sawa na matusi, hivyo anapaswa kuhakikisha kuwa anawaomba radhi wananchi hao kwa madai kuwa amewadhalilisha.
Alisema kiongozi anayepewa dhamana kwa ajili ya wananchi, anapaswa kulinda maslahi ya wananchi wake.
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM), mbali na kudai kushangazwa kauli hiyo ya
Magufuli, alisema hana tatizo na nauli kupanda, isipokuwa mfumo uliotumika kufikia hatua hiyo.
Alisema inashangaza kuona wananchi wanazidi kuongezewa mzigo wa nauli hizo, wakati tayari
mzigo wa kupanda kwa gharama za maisha unawakabili na kudidimiza Taifa kiuchumi.
Kwa pamoja, wabunge hao waliitaka Serikali kushughulikia upungufu uliojitokeza na kama hilo
litashindikana, watapambana na wizara hiyo katika mkutano ujao wa Bunge Dodoma.
Wabunge wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa Umoja huo, Abbas Mtemvu
(Temeke), Mussa Azzan Zungu (Ilala) na wa viti maalumu, Mariamu Kisanji, Zarina Madabida na Philipa Mtulano.
Wabunge ambao hawakuhudhuria ni Makongoro Mahanga (Segerea), Eugen Mwaiposa
(Ukonga) na Halima Mdee (Kawe), Iddi Azzan (Kinondoni).
Juzi Dk Magufuli aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam, kuwa Serikali imeamua kupandisha nauli hiyo kutoka kati ya Sh 50 na Sh 100 hadi Sh 200 kwa safari moja ya kivuko hicho, kutokana na gharama za uendeshaji kuwa juu.
Alisema nauli iliyokuwapo ni ya tangu mwaka 1997 huku nauli za vivuko vingine zaidi ya 30 nchini imekuwa ikipanda mara kwa mara.
Magufuli alisema kivuko cha Magogoni kimekuwa kikitoza nauli za chini ikilinganishwa na cha Chato kinachotoza Sh 300, Pangani Sh Sh 200, Kisorya Sh 300, Lugolola Sh 500, Nyakarilo Sh 300, Chato-Bukombo Sh 2,000, Kirambo Sh 500 na Utete Sh 300; huku wanafunzi wakisafiri bure.
Sambamba na upandishaji nauli kwa watu, pia nauli ya magari imepanda ambapo madogo yanatozwa Sh 800 na Sh 1,500, pick-up Sh 1,000 na Sh 2,000 na yale yenye uzito wa kuanzia tani tatu na nusu Sh 5,000 hadi Sh 7,500.
Juhudi za Magufuli kupatikana azungumzie msimamo huo wa wabunge wenzake, zilishindikana
jana baada ya kufuatwa ofisini kwake na waandishi kuambiwa yuko mkutanoni na hata simu yake haikuwa inapatikana.
1 Comments
hivi haya mapato ya kivuko cha mv, kigamboni yanakwenda wapi????, mbona hakuna kumbukumbu zozote zile zakuonyesha mapato???,pili kwanini zile mashine zilizowekwa pale ferry zimeharibiwa??? jibu ni wizi mkubwa wanaofanya hao wafanyakazi,kwanini waziri magufuli badala ya kuwasidia wananchi wa kigamboni au kuwaeleza hali halisi yeye anawaambia wapige mbizi hivi huyu waziri au kichaa. na hapohapo huyu dewji nae anamtetea waziri.tunajuwa dewji anataka maslahi yake kwa magufuli siyo maslahi ya wananchi walala hoi wa kigamboni,mara tunasikia wanataka kuhamishwa mara nauli bei juu hivi nawauliza hasa nyinyi viongozi kuwa cheo ni dhamana siyo nyinyi wafalme kama mmerithi hii serikali.