Mahakama kuu ya Senegal imetupilia mbali rufaa ya vyama vya upinzani na kuthibitisha kuwa Rais Abdoulaye Wade anaweza kugombea kiti cha urais wa nchi hiyo kwa mara ya tatu.
Upinzani umesema katiba ya nchi hiyo imeweka ukomo wa vipindi viwili, lakini mahakama hiyo imesema Bwana Wade hafungwi na ukomo huo, kwa sababu kwa mara ya kwanza alichaguliwa kabla haijaanza kutekelezwa.
Uamuzi wa kumruhusu Bwana Wade kugombea kwa kipindi cha tatu ulikuwa umezua maandamano nchini Senegal.
Wasiwasi bado umetanda nchini humo baada ya ghasia zilizozuka Ijumaa usiku kufuatia tangazo kwamba Rais Abdoulaye Wade atawania urais kwa mara ya tatu .
Baraza la katiba nchini humo lilimwiidhinisha Bwana Wade, ambaye ana miaka 85, kugombea urais kwa muhula wa tatu lakini ikatupilia mbali ule wa mwanamuziki Youssou N'dour ikisema hakuwa na saini 100,000 zilizokuwa zinahitajika..

Wanaompinga Rais Wade wanasema katiba inaeleza wazi kwamba kiongozi hafai kuwania urais kwa zaidi ya mihula miwili.
Lakini Bwana Wade na wanaomuunga mkono wanasema katiba ilibadilishwa baada ya uchaguzi wa urais na hivyo sheria ya kuwania urais mara mbili tu haimfungi kwa njia yote ile. Anasema sheria hii itatekelezwa kwa marais watakaofuatia.
Wapinzani wake Rais Wade wanasema hajafanya lolote kukabiliana na umaskini katika miaka kumi na miwili ambayo ametawala Senegal, ambako kazi rasmi hazipatikani kwa urahisi. Pia wanasema kwamba hajakuwa na bidii katika kukabiliana na ufisadi.
Lakini Rais Wade amejitetea akisema kwamba chini ya utawala wake, matumizi ya elimu yameongezeka na miundombinu kama vile barabara kujengwa. Anasema hii ni ishara kwamba amefanya juhudi kuhakikisha kwamba Senegal ni kitovu cha biashara.