Na makongoro oging’.
Hakuna mtu anayejutia kuzaliwa, wengi wamekuwa wakifurahia huku wakitegemea maisha mazuri lakini kwa mtoto Mustapha Ali (12) (pichani) imekuwa ni tofauti.
Mtoto huyo ambaye ni mkazi wa Mtoni Mtongani Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam anayesoma darasa la sita ni wa kwanza kuzaliwa katika familia yao na kwa sasa anakabiliwa na mzigo wa kuwauguza wadogo zake mapacha, Swaumu na Ramadhani wenye umri wa miezi nane.
Watoto hao wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mtoto Mustapha ameahidi kuwa atawauguza wadogo zake hadi wapone.
Mustapha, amebaki na jukumu hilo baada ya mama yao aliyekuwa akiwauguza wadogo zake kuugua na kwa sasa yupo mahututi, wakati baba yao alishafariki dunia.
Mtoto huyo anayewauguza wadogo zake katika wadi ya watoto, Makuti B, wiki iliyopita alizungumza na mwandishi wetu na alikuwa na haya ya kusema:
“Maisha yamebadilika ghafla na kuwa mabaya hasa baada ya baba kufariki dunia nikiwa na miaka minne.
“Baba alikuwa akijishughulisha na kazi za vibarua na mama kazi yake ni kuuza mboga mitaani. Kazi hizo zilituwezesha kupata mahitaji ya kila siku na kulipa kodi ya nyumba.
“Mwaka 2007 baba alifariki dunia tukabaki na mama ambaye aliendelea na shughuli na biashara yake. Alikuwa akifanya kazi hiyo bila kupumzika, mzigo wa maisha ulimlemea, nikakatisha kwenda shule nikawa nabaki nyumbani kumsaidia.
“Kufuatia kifo cha baba, muda mwingi mama alionekana mnyonge na aliyejaa mawazo mengi kutokana na kazi ngumu, wakati mwingine alikuwa akitokwa machozi.
“Mwaka juzi mama alipigiwa simu na kuambiwa kuwa bibi anaumwa huko Kigoma na hana mtu wa kumuuguza, ilimbidi aende hata hivyo, hakupona alifia mikononi mwake na baada ya mazishi alirejea Dar na kukuta kodi ya nyumba imeisha.
“Licha ya kusumbuliwa na maradhi, aliendelea na biashara yake kwani hakukuwa na mtu wa kumtegemea, alikuwa akiniambia bila kwenda kwenye shughuli hizo, tungekufa na njaa.
“Mama alianza kuchanganyikiwa kimawazo pale Swaumu na Ramadhan walipoanza kuumwa, alikuwa haendi kuuza mboga. “Maisha yalikuwa ni magumu, tulikuwa tukisaidiwa chakula na wasamaria wema wakati mwingne tulishindia uji.
“Hali za kiafya za wadogo zangu hawa (akiwaonyesha kwa mwandishi), zilianza kuwa mbaya na mama akawa hana fedha za kuwapeleka hospitali.
“Novemba 11, mwaka jana aliamua kuwaleta hapa Muhimbili akiwa hana fedha.
“Alimweleza daktari matatizo yaliyokuwa yakitukabili kiafya na kiuchumi ndipo wadogo zangu walipokolewa na kuanzishiwa matibabu.

“Wadogo zangu walilazwa hapa mimi nilirudi nyumbani na majirani wakawa wanapika huko kwao na kunipa mimi nikawa namletea mama hapa hospitali.
“Niliendelea na zoezi hilo kila siku, nikashindwa kwenda shule lakini niliamini kuwa ipo siku wadogo zangu wangepona nami ningeendelea na masomo.
“Hali ya mama ilizidi kuwa mbaya kuliko hata wadogo zangu akawa anapatiwa, afya yake ilizidi kudhoofu daktari akashauri apewe dawa za kutumia akiwa nyumbani, akarudi nyumbani.
“Hakukuwa na ndugu wa kubaki na wadogo zangu hospitalini, hivyo nikaamua niwauguze, nimekuwa nikilala nao kitanda kimoja.
“Kinachonihuzunisha ni kwamba, sielewi mama anaendeleaje na jambo lingine linaloniumiza kichwa ni kwamba kodi ya nyumba imekwisha mwezi uliopita, sijui tutapata wapi fedha katika hali hii!.
“Mama hana nguvu tena ya kujishughulisha, hatuna ndugu wa kumwangalia ningekuwa na uwezo ningempeleka kwetu Kigoma.
“Nina mawazo mengi kwani hata kama akipatikana mtu wa kubaki na wadogo zangu hapa hospitalini nitaendaje shule? Sina viatu, nguo na madaftari nitaishi wapi na nitakula nini?
“Hata wadogo zangu hawana nguo na mahitaji mengine muhimu.Tunaomba mtu yeyote mwenye huruma atusaidie kutulipia kodi ya nyumba, chakula na nguo ili tuweze kujinusuru na hali ngumu inayotukabili,” alisema mtoto Mustapha huku akitokwa machozi.
Mtu yeyote aliyeguswa na kilio cha mtoto huyo amtembelee Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kama una uwezo, itapendeza ukimsaidia, kwani anahitaji msaada wa hali na mali.