Wajumbe wa chama cha Republican katika jimbo la Florida wamemchagua Mitt Romney(pichani juu) kama mgombea wa chama hicho kupambana na rais Obama katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini marekani baadaye mwezi Novemba mwaka huu.
Huku shughuli ya kuhesabu kura ikikaribia kukamilika Romney ameibuka na ushinda kwa kuzoa asilimia arobaini na sita huku mpinzani wake wa karibu Newt Gingrich akipata asilimia 32.
Kufuatia ushindi huo, Romney(pichani) sasa anaonekana kuelekea kushinda uteuzi wa chama hicho ili kupambana na rais Obama.
Ripoti zinasema Romney alitumia takriban dola milioni kumi na sita kufadhili kampeni za uteuzi huo. Sehemu kubwa ya fedha hizo zilitumiwa katika matangazo ya runinga ambayo yalilenga rekodi ya mpinzani wake mkuu Newt Gingrich ambaye aliibuka mshindi katika uteuzi wa chama hicho katika jimbo la South Carolina.
Hata givyo Gingrich hakufadhaishwa na matokeo hayo akisema kuwa bado kuna majimbo mengine 46 na akaahidi kuendelea na mapambano zaidi.
Matokeo hayo ya jimbo la Florida yamethibitisha kuwa pesa na siasa za kudunisha wapinzani huathiri pakubwa matokeo ya uchaguzi wowote na aliye na fedha nyingi ndiye atakaye kuwa na ushawishi mkubwa.