WABUNGE wawili wamesema bungeni mjini Dodoma kuwa, wanawake wafungwa na mahabusu wanadhalilishwa magerezani kwa kuvuliwa nguo zote, na kurushwa kichura chura wakiwa uchi kama walivyozaliwa.

Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya (CUF), amewaeleza wabunge kuwa, yeye ni shahidi namba moja wa vitendo hivyo akimaanisha kwamba hata yeye alivuliwa nguo zote wakati akiwa mahabusu mkoani Tabora.

Sakaya amewatuhumu maofisa magereza wanawake kuwa wanawadhalilisha wanawake wenzao magerezani na akataka kauli ya Serikali kama ipo tayari kuondoa taratibu za ukaguzi zinazodhalilisha utu wa binadamu.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Balozi Hamisi Kagasheki amelieleza Bunge kuwa hana uhakika kama Mbunge Sakaya alivuliwa nguo akabaki uchi.



Kagasheki amesema, Serikali inalichukulia suala hilo kwa uzito wake na ikithibitika kuna maofisa magereza wanawadhalilisha wafungwa na mahabusu watachukuliwa hatua kali kwa kuwa kuwa mfungwa au mahabusu hakumuondolei mtu haki za binadamu.Wakati anajibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti Maalum, Mhonga Ruhwanya (Chadema), Kagasheki alisema, yupo tayari kufuatilia ili kupata ukweli wa tuhuma hizo na hatua zinazostahili zitachukuliwa bila mashaka wala kigugumizi.

Wakati anauliza maswali hayo , Ruhwanya alionesha kutokubaliana na majibu aliyotoa Kagasheki wakati anajibu swali la msingi lililohusu udhalilishwaji wa wafungwa na mahabusu wanawake katika Gereza la Bangwe mkoani Kigoma.

Mbunge huyo amedai kuwa, kuna matendo ya ukatili na uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu wanawake katika magereza nchini ikiwa ni pamoja na kwenye gereza hilo.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wanawake wafungwa wanapoingia magerezani wanavuliwa nguo zote na kupewa adhabu ya kuruka kichura wakiwa kama walivyozaliwa.

Alitaka Serikali itoe tamko kali kwa kuwa ushahidi uliopo si wa picha, ni wa moja kwa moja na pia akataka Seriali iseme itawachukulia hatua gani askari magereza wa Gereza za Bangwe kwa kuwa wanawadhalilisha wanawake na wameidanganya Serikali.

Kagasheki amelieleza Bunge kwamba, ni mara ya kwanza Wizara kupata taarifa hizo za kushtua kuhusu Gereza la Bangwe.

“Tumefuatilia bila kupata ushahidi wa jambo hili. Namuomba Mheshimiwa Mbunge kama anao ushahidi wa jambo hili anipatie mara moja” amesema Kagasheki wakati wa kikao cha pili cha Mkutano wa Sita wa Bunge la 10.

“Bila kuwabaini askari wanaofanya vitendo hivyi ni vigumu kuwaadhibu kama aelezavyo Mheshimiwa Mbunge” amesema Kagasheki.

Amesema, kuna kanuni na taratibu zinazofuatwa zinazolinda na kuthamini haki za utu wa wahalifu wanapoingia na wanapokuwa magerezani chini ya kanuni za kudumu za uendeshaji wa Jeshi la Magereza za mwaka 1968.

“Kanuni hizi hazimruhusu askari kutothamini au kumdharau au kumdhalilisha mfungwa na kumtesa mfungwa”amesema Kagasheki.
                                                 CHANZO