Na Khatimu Naheka
KIKOSI cha Yanga kimeondoka jana jijini Arusha kurejea Dar es Salaam kikiwa kimeacha deni katika Hoteli ya Jeshmark huku kiongozi mmoja wa klabu hiyo akishikiliwa na uongozi wa hoteli hiyo.
Yanga ilikaa katika hoteli hiyo kwa siku tatu ikijiandaa kuivaa JKT Oljoro kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kumalizika kwa vijana hao wa Jangwani kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Championi Ijumaa kuwa awali kikosi hicho kilitaka kuondoka bila kulipa kwa madai kuwa kitafanya hivyo kikifika jijini Dar es Salaam, lakini uongozi wa hoteli ukakataa na kutaka meneja wa timu abaki.
“Walitaka meneja wa timu, Hafidh (Saleh), abaki mpaka deni hilo litakapolipwa. Hivyo, kiongozi huyo amebaki akisubiri viongozi watume fedha hizo,” kilisema chanzo hicho.
Ofisa Habari wa yanga, Louis Sendeu alipoulizwa juu ya hilo alisema: “Sijapata taarifa kuhusiana na suala hilo.” Naye katibu wa timu hiyo, Selestine Mwegwa, alisema bado hajapata taarifa na alikuwa akingojea timu iwasili jijini kisha ndiyo atatoa taarifa rasmi.