RAIS Jakaya Kikwete, amewasilisha kwenye Kamati Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), taarifa yenye azma ya kulipanga upya Baraza la Mawaziri ili kuwawajibisha Mawaziri waliotajwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusika na ubadhirifu wa rasilimali za umma.

Pamoja na Baraza la Mawaziri, Rais Kikwete katika taarifa hiyo kwa Kamati Kuu, ameeleza pia nia yake ya kupangua watendaji wakuu wa Wizara wakiwemo Makatibu Wakuu na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, waliotajwa pia na CAG kuhusika na ubadhirifu huo.

Kutokana na kuibariki taarifa hiyo iliyowasilishwa na Rais Kikwete kwa Kamati Kuu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete ameshauriwa na Kamati hiyo kulisuka Baraza hilo mapema iwezekanavyo.
Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Taifa, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kwamba pamoja na taarifa hiyo ya Rais, Kamati Kuu pia ilipokea na kuzijadili taarifa na maazimio ya Kamati ya Wabunge wa CCM na Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM juu ya kilichotokea kwenye Bunge lililomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

“Pamoja na taarifa hizo Kamati Kuu imepokea taarifa ya jinsi Rais alivyojipanga kuchukua hatua za kuwawajibisha Mawaziri na Watendaji wa Serikali na wale wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali, Kamati za kudumu za Bunge na wabunge bungeni, “ alisema Nape.

Alisema Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa serikali yao na inapongeza juhudi za serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua mapungufu yaliyojadiliwa na Bunge hilo.

Kwa mujibu wa Nape, Rais Kikwete pamoja na kuhudhuria sherehe za Muungano, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi mchana, ambaye alimpatia taarifa ya kile kilichotokea bungeni Dodoma hadi kufikia hatua ya Kamati ya Wabunge wa CCM, kuwataka Mawaziri waliotajwa kwenye taarifa ya CAG kuwajibika.

Alichukua nafasi hiyo kupuuza taarifa za chini kwamba kambi ya upinzani bungeni ndiyo iliyosababisha shinikizo hilo, akisema taarifa ya CAG imeweza kupelekwa na kujadiliwa bungeni kutoka na mfumo aliouasisi Rais Kikwete wa kutaka taarifa ya CAG kuwa wazi zaidi kuliko ilivyokuwa awali ikiwa ni pamoja na kupelekwa bungeni kwa uwazi ili kujadiliwa.

“Hili ni vizuri likafahamika. Rais hajaishia hapo tu, hata ule mfumo wa maofisa wa CAG kuwa na ofisi kwenye majengo ya serikali kama kwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) sasa haupo. Rais ameweka mfumo ambao wakaguzi hawa sasa wanakuwa na ofisi nje ya majengo ya serikali ili wanapokuja kuwakagua watendaji wa serikali wawe huru,” alisema Nape.



Ingawa Nape hakuwataja lakini katika kikao cha Bunge kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Mawaziri saba walibanwa na Wabunge wa CCM wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu na hivyo kukididimiza chama hicho kisiasa.

Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo alituhumiwa na wabunge wengi kuwa si mwadilifu na
anaongoza kutumia fedha za umma. Mkulo pia alituhumiwa kuuza mali za Serikali kiholela bila kulishirikisha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC). Ripoti ya CAG ya mwaka uliopita wa fedha imetoa mifano ya viwanja vilivyouzwa na Mkulo bila kuishirikisha CHC.

Waziri mwingine ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda ambaye wizara yake inatuhumiwa kutumia Sh bilioni moja kwenye Maonesho ya Nane Nane. Mwingine ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami na Naibu wake Lazaro Nyalandu ambao wanatuhumiwa kumlinda Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango (TBS).

Kwenye orodha hiyo yumo Waziri Jumanne Maghembe ambaye ni Waziri wa Kilimo anayeelezwa kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji wa bodi ya Pamba ambao wametafuna Sh bilioni 2 zilizotolewa na Serikali kuwalipa wakulima wa zao hilo baada ya kutokea mdororo wa uchumi.
Pia yumo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye wizara yake imetajwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa imegubikwa na rushwa katika ununuzi wa mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura.

Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika ambaye wizara yake kwenye taarifa ya CAG
imeonesha kufanya madudu kutokana na ulaji uliokithiri kwenye halmashauri za wilaya anashutumiwa kushindwa kuchukua hatua kwa watendaji wa chini yake badala yake amekuwa anawahamisha vituo vya kazi wabadhirifu hao.

Habari hizo pia zilimtaja Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye wizara
yake imegubikwa na kashfa ya majangili kuua tembo wengi mwaka jana kuliko wakati
wowote ule kuwahi kutokea. Utata wa ugawaji wa vitalu vya kuwindia pia ni kashfa
ambayo imekuwa inaitafuna wizara hiyo kwa muda mrefu. Nape hakusema kama Mawaziri hao wataguswa na fagio hilo la Rais Kikwete au la.

Nape alisema pamoja na Mawaziri hao waliotajwa, Rais anaweza kuchukua mwanya huo kuwapangua Mawaziri na watendaji wengine wa serikali anaoona mchango wao katika kuiendesha serikali umekuwa mdogo kuliko anavyohitaji.

Mbali ya hilo, Nape alisema Kamati Kuu imeipongeza Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyoundwa kuchunguza utendaji katika sekta mbalimbali kwenye serikali ya Mapinduzi Zanzibar na imewapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa jinsi walivyojadili taarifa hiyo na imeipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuipokea taarifa hiyo na kuanza kuifanyia kazi.

Katika hatua nyingine Kamati Kuu ya Taifa ya CCM, imewateua wanachama wake watano kuwa Kaimu Makatibu wa Mikoa wa chama hicho baada ya serikali kuunda mikoa mipya mitano ya Geita, Njombe, Simiyu, Katavi na Mjini Magharibi, Zanzibar.
Nape aliwataja walioteuliwa kuwa ni Hilda Kapaya, Shaibu Akwilombe, Hosea Mpagike, Alphonce kinamhala na Aziz Ramadhan Mapuri, ambao vituo vyao vya kazi vitatajwa baadaye.