Ndugu
Wananchi,
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa
kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama.
Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda
kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa
binadamu nchini na la pili ni la mgomo wa madaktari.
Usafirishaji
Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu
Wananchi;
Bila
ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la
kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka
kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni,
2012. Pamoja na maiti hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote
wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa
kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa
Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika
Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na
21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia
wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini
ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. Kwa
mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita. Mwezi mmoja
waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha
ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini
ikaishia Chitego. Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo
kusababisha vifo kwa kukosa hewa.
Tukio
la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa wamekufa si
la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika kipindi cha takriban miaka 10
sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji haramu kuingia nchini. Kwa mfano,
kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla ya wahamiaji haramu 19,683
wamekamatwa. Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu
1,500 tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao.
Wengi wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na
Bangladesh.
Wahamiaji
haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi. Wapo wanaotumia
nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Na, wapo
wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja na za mikoa ya ukanda wa
Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani, Lindi na
Mtwara.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini kuhamia bali
wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako wameahidiwa kuwa
watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya. Watu hao pia
wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na usafiri wao tangu nchi
watokako na zote wanazopitia mpaka kule waendako. Aidha, wamesema kuwa wao
wanawalipa watu hao ili wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni
kwamba hili si suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya
kusafirisha binadamu.
Ndugu
Wananchi;
Kufuatia
vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo wasafirishaji
walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo. Makontena, malori yaliyofunikwa
nyuma na matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa yanatumika kwa ajili hiyo.
Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26
Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani
Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa
wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini
kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu na hasa mbinu
mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa vyombo vya dola kwa kazi
nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara hii haramu hapa nchini.
Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti huo kwa lengo la kukomesha kabisa
biashara hii.
Niliagiza
pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi sasa
kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa pamoja
tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia, Kenya, Malawi,
Msumbiji na Afrika ya Kusini kutambua mawakala na kuwabana kwa mujibu wa
sheria. Tayari nimeshaanza kufanya mawasiliano na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo
kuhusu ushirikiano huo. Nashukuru wote wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa
pamoja kuvunja mtandao huu mchafu na kutokomeza biashara hii haramu na
inayodhalilisha utu wa mwanadamu.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego na Mkoka
kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha uzalendo wa hali ya
juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe, lakini pia wameonesha utu kwa
kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili. Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa
Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa
kulishughulikia tatizo hilo kwa umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na
ushirikiano ulioonyeshwa na vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika
kushughulikia suala hili.
Mgomo
wa Madaktari
Ndugu
Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi sasa.
Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee tarehe
12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa unaendelea wakati ule pamoja
na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua iliyokuwa imefikiwa, nilielezea
mazungumzo yangu na viongozi wa Chama cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa
Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo
na watarudi kwenye meza ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea
matumaini yangu kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya
matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa
wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma wanazostahili
kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu
Wananchi;
Kama
walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi kwenye
mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi
tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka
2004. Chama cha Madaktari na Serikali walifika katika Tume ya Usuluhishi na
Uamuzi (Commission for Mediation and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa
pamoja na kwa ridhaa yao wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa
ya kuzungumza wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano
yao. Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8 Machi,
2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja na kuagiza
kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu
Wananchi;
Kati
ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao sita vya
majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari. Katika mazungumzo hayo
hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo ni haya
yafuatayo:
1.
Posho
ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya
mshahara.
2.
Posho
ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia
30 ya mshahara.
3.
Madaktari
wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya
mshahara.
4.
Posho
ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya
mshahara.
5.
Madaktari
walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe
magari.
6.
Madaktari
wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa
mwezi.
7.
Madaktari
wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8.
Hatua
za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii.
9.
Viongozi
wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10.
Madaktari
waliofukuzwa warudishwe kazini.
11.
Huduma
za afya ziboreshwe nchini.
12.
Posho
ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu
Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa
pamoja kwa mambo saba. La kwanza, ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi
kazini. Serikali ilieleza kuwa upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi
wa Serikali Na. 3 wa mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za
kununulia magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa
madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la pili, ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya.
Jambo hili lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za
utekelezaji wake.
Jambo la tatu, ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya
Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo
liko nje ya mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za
uteuzi. Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.
Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka waonane
kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni sababu kwa vile
wameyazungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya
mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa
ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza, kwamba maelekezo
ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari wazingatie maadili ya kazi zao
na kukataa kutoa rufaa kwa mtu asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi.
Pili, walikubaliana kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi
watibiwe hapa nchini. Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali.
Nililieleza hili mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge
baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza
sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi
shilingi trilioni 1.2 mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya
miundombinu na elimu. Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na
wataalamu wa afya. Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza
katika Hospitali ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka
sita nyuma. Na kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa
nje. Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa na
mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu. Tunaendelea
kuimarisha mafunzo ya madaktari na madaktari bingwa, yote kwa nia hiyo hiyo.
Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili kinachukua wanafunzi wengi
zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa
ili kuchukua wanafunzi wengi zaid. Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa
46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu
Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari
waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa Wizarani
kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na
Lugalo. Hili ni jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa
wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari
kuhusu kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na
mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya bajeti ya
Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na kuboresha viwango
vya ubora wa madaktari na kadhalika. Serikali imeyaafiki mapendekezo hayo na
yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho
ya uchunguzi wa maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo,
Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi
kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa
wasaidizi wake.
Ndugu
Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na
kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali imekubali hoja ya kuchukua hatua ya
kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi. Serikali
iliwaeleza kuwa watumishi wa kada zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya
maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha,
Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa
watumishi wa umma wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada ya uchambuzi
wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango stahiki viwe vipi na
nani hasa wahusike. Madaktari wamekataa hili la kufanya uchambuzi, wanataka
kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na
kianze mara moja.
Jambo la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi.
Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za kuishi. Aidha,
imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini
na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa
wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa
maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema waajiri
wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma
wenye stahili ya kupewa nyumba. Jambo hilo limekataliwa na Madakari na kutaka
lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba. Serikali
kwa upande wake imeona vigumu kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa
wafanyakazi wengine wote wa umma.
Jambo lingine ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho
ya kufanya kazi katika mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa
yapo baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma
hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali wajibu wa
kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika maeneo hayo. Kwa ajili
hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za ajira kuhusu namna ya kuwasaidia
watumishi hao kupunguza makali ya maisha katika kila eneo badala ya kutegemea
posho peke yake.
Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila
itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua
watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali
ilipe posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali ni rai ya
Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho
kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya
hayo.
Ndugu
Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili. Jambo la
kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza sina budi kueleza
kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu Februari, 2012 posho
iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi 25,000/= kwa
daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili
wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/= kwa madaktari waliohitimu
ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini (Interns). Viwango hivyo vya posho
vinatumika hivi sasa.
Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza
walipwe asilimia 10 ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari
ni kuwa sharti la malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha
mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na
hakutokea aendelee kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya. Linaweza
kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile wana hakika
mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu
mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe shilingi
3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali
imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka
20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa
fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya
shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi
hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi
3,500,000/=.
Ndugu
Wananchi;
Huo
ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo ya
mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30 Mei, 2012,
upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya nyongeza ya mshahara
haina mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na majadiliano mpaka
watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi kutoa taarifa ndani ya wiki mbili.
Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT aliandika barua kwa Katibu Mkuu Utumishi
ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa upande wa Serikali, kuwa Madaktari
wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu
Wananchi;
Baada
ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na Madaktari
walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro umekosa usuluhishi
kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili zilikubaliana suala hilo
lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi. Wakati pande zote zinasuburi mgogoro
huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu, upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa
mgomo kuanzia saa sita ya usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili
kwani suala lenyewe halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za
Mahusiano ya Kazi nchini.
Ndugu
Wananchi;
Tarehe
22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu Kitengo cha
Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la muda kufanywa.
Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo usitishwe. Juhudi za
kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na viongozi wengine wa MAT
hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa na simu zote za viongozi wa MAT
zilikuwa zimezimwa. Hatimaye tarehe 25 Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri
hiyo ya Mahakama. Tarehe 26 Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo
alikana kuwa yeye hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika.
Pamoja na rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake
kusitisha mgomo. Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo umekuwa
unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu
Wananchi;
Wagonjwa
wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali kisheria
ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari. Viongozi wa
MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika mgogoro na Mahakama na waajiri wao
isivyostahili. Ni vyema viongozi wa Madaktari na madaktari wakatambua kuwa
wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana
Mahakamani kuwa hahusiki nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao
wanaziweka hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa
kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana pa
kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns, wanahatarisha maisha
yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki mgomo usiokuwa halali.
Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu
Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa kuboresha
mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu kwa maelekezo ya
Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo sera hiyo, hata hivyo ni
ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee haitoshi, lazima uwezo wa kufanya
hivyo uwepo. Kwa kulingana na uwezo uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na
maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya
hivyo kwa jumla kwa wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa
umma.
Miongoni
mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni madaktari na
watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya. Tena nadiriki kusema madaktari
tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi wengine wa umma. Upendeleo upo
kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa
asilimia mia moja wakati wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako
hivyo.
Ndugu
Wananchi;
Mwaka
2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=,
mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea
kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/= wanazolipwa
sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi wa taaluma nyingine
wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa wastani hupata shilingi
446,100/=.
Tunafanya
hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii na
ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari nchini.
Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu
Wananchi;
Sina
budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio nao wa
kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa kuwalipa mshahara wa
kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo
malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=. Kwa
hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu
tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana
na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini
bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda kwa muajiri
anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila la heri. Hana sababu ya
kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo.
Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo
wa kumlipa anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia
barua ya kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua
hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa
kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa
kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana jinsi bali kukuondoa
kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na maadili ya kazi ya
udaktari.
Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya hivyo kwa
wote wanaoendelea kugoma. Najua baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna
manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya
hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo
ajae awe na mahali pa kuishi. Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari
ambae hayupo kazini na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi wa
umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya hivyo, na tutaendelea
kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni vyema watumishi wa umma
wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au kiasi kikubwa mno cha pesa za
umma kulipana mishahara. Tukifanya hivyo, Serikali itashindwa kutoa huduma
muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo
huduma za afya tunazosema ni duni tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama
tutatumia sehemu kubwa ya pesa za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi
sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango
hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi
asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na
shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa
asilimia 13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio
wengi.
Suala
la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu
Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote kuelezea
masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha kinyama
alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni, 2012. Kitendo hicho
ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu. Watanzania hatujayazoea mambo hayo.
Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili
ukweli ujulikane. Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili
tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi
sasa.
Natambua
kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi
nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya hivyo.
Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali
na Madkatari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo hakustahili
kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini
nilisema wamuache maadam Madaktari wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri
zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na Serikali.
Ndugu
Wananchi;
Kama
nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa yamepatikana.
Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo hatukuweza kukubaliana.
Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria
kusaidiwa. Kwa nini Serikali imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama
Kuu imekwishatoa amri ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua
ugomvi na mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu
huyo. Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven Ulimboka
kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna mtu wa Serikali
kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na
Serikali.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt. Steven
Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na Watanzania
wenzake katika ujenzi wa taifa. Kwa namna ya pekee namshukuru na kumpongeza
Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na upendo na kwa hatua alizochukua za
kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba
kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini. Watanzania
wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa huruma na upendo na
msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Asanteni kwa
Kunisikiliza
|
0 Comments