Moses Ng’wat, akiagana na mzee Nyimbo mara baada ya mkutano na waandishi wa habari wa mbeya na Iringa
TUKIO la kuuawa kwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi, limeendelea kuibua mambo mapya, baada ya aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo la Njombe Magharibi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kudai chama chake kilishiriki mauaji hayo kwa asilimia 50 na asilimia nyingine 50 ilifanikishwa na Serikali kupitia Jeshi la Polisi.
Nyimbo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wandishi wa Habari Jijini Mbeya katika mkutano wake aliouandaa kwa nia ya kutangaza nia yake ya kujiuzulu uanachama wa Chadema na kubakia mwanasiasa huru asiye na chama.
Alisema kuwa Chadema hawakuwa na sababu ya kwenda kuzindua tawi la chama hicho katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi kwa sababu tawi hilo alikuwa tayari alishalizindua yeye mwenyewe miezi mitatu kabla ya kutokea kwa mauaji ya marehemu Mwangosi.
“Asilimia hamsini, mauaji ya rafiki yangu Marehemu Mwangosi yalisababishwa na Chadema kwa kutotii amri ya Jeshi la Polisi na kupanga kwenda kuzindua tawi la chama ambalo mimi nikuwa tayari nimekwishalizindua miezi mitatu iliyopita kabla ya tukio lile,” alisema Nyimbo.
Nyimbo alisema kuwa tabia ya viongozi wa kitaifa wa Chadema kutoka makao makuu ya Chama Jijini Dar es Salaam na kwenda mikoani kufanya mikutano ambayo huwa haijafanyiwa maandalizi yoyote na wenyeji wao, hali ambayo inawafanya walazimike kufanya maandalizi wao wenyewe, ndiyo inayosababisha migongano isiyokuwa ya lazima na Jeshi la Polisi na hatimaye kuwa chanzo cha vurugu kwenye mikutano ya chama hicho.
Alisema kuwa kwa kawaida mikutano ya siasa inapaswa kuandaliwa na wenyeji kwa kuwa ndio ambao wanaofahamiana vizuri na uongozi wa Jeshi la Polisi katika eneo husika kwa kuwa wao wakikaa na kuzungumza huelewana, lakini suala hilo linapoingiliwa na wageni husababisha viongozi wa sehemu husika kuwa na wasiwasi wa usalama na hivyo kutokea migongano inayosababisha kutokea kwa vurugu.
Akizungumzia ushiriki wa Jeshi la Polisi katika mauaji ya Mwangosi, Nyimbo alisema kuwa haikuwa sahihi kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (RPC), Michael Kamuhanda kuingilia kati suala hilo kwa kuwa sheria ya mikusanyiko inaeleza wazi kuwa mwenye jukumu hilo ni Mkuu wa Polisi wa eneo linalofanyika tukio ambaye alipaswa kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).
Alisema kuwa ikitokea OCD akazidiwa nguvu au kushindwa kutoa maamuzi kwa suala husika ndipo hulazimika kuomba msaada kwa bosi wake ambaye ni RPC ambaye naye anastahili kutoa maelekezo na sio kwenda moja kwa moja kwenye eneo la tukio kama alivyofanya Kamuhanda.
Kwa mujibu wa Nyimbo, hata tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kuchunguza chanzo cha mauaji hayo ilikuwa ni batiri kwa sababu Dk. Nchimbi ni sehemu ya watuhumiwa kwa upande wa Serikali.
Alisema kilichotakiwa kufanyika baada ya kutokea kwa tukio hilo ilikuwa ni uwakamata viongozi wote wa Chadema na viongozi wa Polisi waliokuwa eneo la tukio na kuwaweka ndani kwa muda kupisha uchunguzi wa tukio hilo na pia kuwapa fundisho wasijaribu kuchezea roho za watanzania na amani ya taifa.
Mwangosi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC) aliuawa kwa kulipuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu wakati akiwa kazini katika kijiji cha Nyororo wilayani Mufindi ambako Chadema walikuwa wakizindua tawi la chama hicho kijiji hapo.
Na Moses Ng’wat,Mbeya. picha na Mbeya yetu
|
0 Comments