MWIGIZAJI Nyota katika tasnia ya filamu Swahiliwood, Yvonne Cherryl Monalisa(pichani kishoto) amewashutumu wasanii wenzake kwa kusema uongo katika jamii kuhusu maisha yao halisi pamoja na malipo wanayopata.
Binti huyo amedai kwa kufanya hivyo wasanii wengi wemejikuta katika maisha ya kuunga unga kutokana uongo huo.
Baadhi ya wasanii wa filamu wanadanganya sana kuhusu hali halisi ya maisha yao, mtu akipata nafasi ya kuongea na vyombo vya habari kuhusu malipo na maisha yake halisi utakuta akisema kuwa yeye bila kulipwa milioni tano hawezi kushiriki katika filamu, lakini ukweli hakuna msanii wa kawaida anayelipwa fedha kama hizo katika tasnia ya filamu Bongo mimi mwenyewe ni mtayarishaji, anasema Monalisa.
Anaendelea kudai kuwa kutokana na udanganyifu huo Serikali kupitia Bodi ya Filamu iliamua kuongeza gharama za kibali cha kurekodi filamu hadi kufikia Shilingi 500,000 jambo lilofanya wasanii walalamike kama ni fedha kubwa sana kulingana na malipo ya filamu, lakini ilitokana na udanganyifu kutoka kwa baadhi ya wasanii wa filamu kudanganya, mwanadada huyo anasema hali ya soko la filamu ni mbaya kwa sasa.