Wafanyakazi katika mataifa kadhaa ya muungano wa Ulaya wameandamana na kufanya migomo kupinga kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na mikakati ya serikali ya kupunguza matumizi yake.
Migomo hiyo nchini Uhispania na Uturuki imekwamisha shughuli za usafiri, biashara na shule na maafisa wa polisi wamekabiliana na waandamanaji hao katika mji mkuu wa uhispania Madrid.


Kumekuwepo pia na maandamano katika mataifa ya Ugiriki, Italia na Ubelgiji na maandamano mengine yanatarajiwa katika mataifa mengine.
Safari za ndege nchini Uhispania na Ureno zimefutwa ambapo mashirika ya ndege yametoa wito kwa wasafiri kuchunguza ratiba ya usafiri kabla ya kuelekea katika viwanja vya ndege.
Migomo hiyo imeandaliwa na Chama cha wafanyakazi barani Ulaya ETUC ambacho ndicho kinaongoza migomo hiyo inayotarajiwa kushuhudiwa katika mataifa yote ya ulaya.
Mratibu wa chama hicho Judith Kirton-Darling ameiambia BBC kuwa mipango ya kupunguza matumiza ya serikali haifanyi kazi kwa kuwa raia wa kawaida ndio wanaoendelea kuteseka.
Jumla ya makundi 40 kutoka mataifa 23 yamehusika na maandamano yaliyofanyika hii leo.
Vyama vya wafanyakazi nchini Uhispania na Ureno vilitangaza kuwa mgomo huo ambao ulianza saa sita za usiku kupinga mipango ya serikali zao ya kupunguza matumizi , kuongezwa kwa viwango vya ushuru, mishahara ya wafanyakazi, malipo ya uzeeni pamoja na huduma zingine zikipunguzwa.