RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, zitaendelea kushirikiana katika kuendeleza na kuulinda muungano ulioipatia sifa Tanzania kutokana na kuimarika kwake.
Dk Shein aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Aman mjini Zanzibar.
“Muungano wetu upo imara na umepata heshima kubwa sana katika mataifa mbalimbali, Serikali zetu mbili zitaendelea kushirikiana katika kuendeleza muungano wetu na kamati za pamoja za kushughulikia kero za muungano, zitaendelea kuyapatia ufumbuzi yale ambayo wameanza kuyashughulikia,” alisema Dk Shein.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilali, Dk Shein alisema kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa mfano wa kuigwa, ndani na nje ya nchi kutokana na mafanikio yaliyofikiwa kiuchumi na kisiasa.
“Muungano huu umekuwa chachu ya maendeleo kwa Wazanzibari, ndiyo maana Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaendelea kuudumisha. Nafahamu kuna changamoto  za Muungano, ambazo Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano inazishughulikia. Tunachotakiwa ni kuendelea kuudumisha, ili ushirikiano wetu uzidi kuwa imara kwa faida na maslahi ya Watanzania wote,” alisema Dk Shein.
Dk Shein pia aliwakumbusha wananchi umuhimu wa mapinduzi yaliyotokea Januari 12, 1964, akisema mapinduzi hayo yamerudisha utu na heshima ya Wazanzibari, ambao sasa wanaishi kwa mshikamano na maelewano.
Dk Shein aliwataka wananchi wote wa visiwa hivyo kufanya kazi kwa bidii, ili kujiletea maendeleo kama sehemu ya kumuenzi Mzee Abeid Amani Karume na waasisi wengine wa mapinduzi hayo.
Alisema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli za kimaendeleo ili kujenga uchumi imara wa Zanzibar.
“Tuna changamoto nyingi za kimaendeleo. Vijana wetu wengi hawana ajira, lakini Serikali itahakikisha inawapatia mikopo na mafunzo kupitia vikundi vyao, ili waweze kushiriki katika uzalishaji mali. Pia wajasiriamali nao tutajitahidi kuwawezesha ili kuongeza tija katika shughuli zao za kimaendeleo,” alisisitiza Dk Shein.
Mafanikio ya Serikali
Akizungumzia mafanikio Dk Shein alisema kwamba Serikali yake imepata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, elimu na miundombinu, huku akiwahakikishia Wazanzibari kuimarika kwa upatikanaji wa maji na umeme katika kipindi kifupi kijacho.
Dk Shein alisema ukuaji wa uchumi unatazamiwa kufikia asilimia saba kutoka asilimia 6.8 katika mwaka 2011, huku pato la taifa likiongezeka kwa Sh1,198 bilioni katika mwaka 2011 kutoka Sh946.8 bilioni katika mwaka 2010.
Alisema kuwa mafanikio hayo ya kukua kwa uchumi yamesaidia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa mbalimbali za chakula kutoka asilimia 20.8 Desemba mwaka 2011, hadi 4.2 Novemba mwaka 2012  na kutoa faraja kubwa kwa wananchi.
Rais huyo wa Awamu ya Saba wa Zanzibar alisema kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kutoka Sh181.4 bilioni mwaka wa fedha 2010-2011 na kufikiya Sh212 bilioni  katika mwaka 2011-2012,ikiwa ongezeko la asilimia 17.