Barua hiyo ya tarehe 28 Novemba, 2012 ilisema kuwa
hoja hiyo ya Zitto ni ya uongo, imemkashifu mteja wao na kumshushia
hadhi yake binafsi na biashara zake.
“Katika kuthibitisha kuwa tuhuma zako siyo za kweli katika hoja
uliyotoa, umemtaja mteja wetu kama raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo. Mteja wetu ni raia wa Afrika Kusini, lakini, umeamua kumtaja kama
raia wa Kongo bila kuangalia ukweli,” alisema Shein.
Katika barua hiyo, Shein pia amesema kuwa Zitto
amemtuhumu mteja wake Mabanga kuwa aliwahonga baadhi ya vigogo
serikalini na kuwapa rushwa wanasiasa katika mchakato wa kufanikisha
upatikanaji wa vitalu hivyo.
“Tuhuma hizo siyo za kweli, mteja wetu alifuata
taratibu zote kwa uwazi na mamlaka husika nchini na hakuwahi kutoa
rushwa kwa mtu yeyote,” alisema mwanasheria huyo.
“Tuhuma hizi ni za uongo, zimemharibia jina mteja
wetu na kumsababishia madhara. Kama hutazifuta kauli hizo, uongo huo
utamsababishia mteja wetu madhara makubwa zaidi na tutalazimika kudai
fidia,” Shein alionya kupitia barua hiyo.
Shein aliongeza kuwa pamoja na Zitto kuongea hoja
hiyo akiwa bungeni hivyo kuwa na kinga ya kibunge, lakini kwa mazingira
aliyotolea hoja hiyo alitumia vibaya kinga ya kibunge, anayopata mbunge
yeyote anapotoa hoja akiwa bungeni.
Kupitia barua hiyo, Shein alimtaka Zitto kufuta
kauli yake dhidi ya mteja wao na kwamba mteja wao ana haki zote za
kushtaki dhidi ya hoja hiyo.
Zitto azungumza
Alipotakiwa
kuzungumzia hoja hiyo na hatua atakazochukua, Zitto alisema kuwa
amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, kumjulisha
hatua hiyo ya kutaka kushtakiwa.
“Nimemwandikia Katibu wa Bunge
kumjulisha kwamba nimeletewa kusudio la kushtakiwa, maana hili ni suala
la Kinga ya Bunge,” alisema Zitto na kuongeza:
“Mbunge ana kinga kwa masuala aliyozungumza ndani
ya Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba. Kwa hiyo Katibu (Dk
Kashililah), atawajibu hao wanasheria.”
0 Comments