ABIRIA 25 waliokuwa wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam wamenusurika kufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kupata ufa katika kioo cha mbele, hivyo kumfanya rubani abadili mwelekeo na kutua kwa dharura uwanja wa ndege wa Kigoma.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni muda mfupi baada
ya ndege hiyo aina ya Bombadia Dash 8 kuruka katika uwanja wa ndege wa
Kigoma, ikiwa katika safari zake za kwanza, baada ya kusitishwa takriban
miezi tisa iliyopita.
ATCL ilisitisha safari zake April 9, 2012 baada ya
ndege yake aina ya Dash 8 kupata ajali katika kiwanja cha Kigoma, hivyo
Shirika hilo kukosa ndege nyingine. Miezi miwili iliyopita shirika hilo
lilinunua ndege mpya.
Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro alisema ilipata
hitilafu hiyo dakika 15 tangu iliporuka, baada ya kioo cha mbele kupata
ufa.“Ufa ule uliwatisha marubani na waliamua kutua kwa dharura kwa
sababu kioo kingeweza kupasuka na kusababisha ajali mbaya na ndege
kuanguka,” alisema Lazaro na kuongeza;
“Kawaida vioo vya ndege hupashwa moto ndege
inapoondoka na endapo utatokea ufa wowote ni lazima irudi kiwanjani na
kama ipo mbali na kiwanja inambidi rubani ateremke chini na kupunguza
mwendo.”
Alisema kutokana na hali hiyo, wapo kwenye
harakati ya kuifanyia matengenezo ndege hiyo na wakati wowote itarudi
kwenye safari zake za kawaida.
0 Comments