Wanajeshi wa Nigeria wamesema wamemtia
nguvuni kiongozi mmoja wa kundi la wapiganaji wa Boko Haram kaskazini
mwa nchi hiyo.
Taarifa zinadokeza kuwa Kiongozi huyo Mohammed Zangina alitiwa nguvuni katika Mji wa Maiduguri.
Wanajeshi hao wanadai Zangina alihusika kupanga mashambulizi ya kujitolea muhanga katika Miji kadhaa.
Jeshi la Nigeria lilikuwa limetangaza zawadi ya dola laki moja na sitini kwa yeyote atakayemkamata kiongozi huyo.
Kikosi maalum cha jeshi kilisema kilimkamata
Zangina mapema Jumapili katika mtaa mmoja wa kifahari mjini Maiduguri
ambako ndio ngome ya harakati za Boko Harama.
Hata hivyo duru zinasema kuwa jeshi la Nigeria
wakati mwingine huongeza chumvi madai yake kuhusiana na kundi hilo
ambalo limehusika na mashambulizi kadhaa Kaskazini mwa nchi.
Taarifa ya jeshi ilisema kuwa alikuwa mjini Maiduguri kupanga mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama
Likitaja miji kadhaa nchini humo, jeshi lilisema
kuwa Zangina ndiye amekuwa akiongoza mashambulizi katika miji hiyo
ikiwemo Abuja, Kaduna, Kano, Jos na Potiskum."
Jeshi limekuwa likidai kuwakamata vigogo wa
kundi hilo katika miezi ya hivi karibuni ingawa hakuna uhakika ikiwa
Boko Haram imeathirika kwa vyovyote. |
0 Comments