Takriban watu 17 wamethibitishwa kufariki baada ya jengo walimokuwa kuporomoka mjini Dar es Salaam hapo jana asubuhi.
Kamimishna wa polisi Saidi Meck Sadick alisema watu 21 walinusurika kifo.
Aliongeza kuwa wangali wanawatafuta manusura.

Ripoti za mapema zilisema kuwa watu 45 ikiwemo wafanyakazi wa mjengo na watoto wa shule ya mafunzo ya dini ya kiisilamu bado hawajaptikana.

Mwandishi wa BBC Hassan Mhelela anasema kuwa jengo hilo limeharibiwa vibaya sana na kuwa lilikuwa liwe jengo na ghorofa kumi na mbili lakini wajenzi walikuwa wamejenga hadi ghorofa 16.


Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo Nishit Surelia, aliambia BBC kuwa "tulisikia sauti kubwa na kisha jengo likaporomoka. Kila mtu alianza kukimbia wakifikiria kuwa lilikuwa tetemeko la ardhi . Vumbi lilikuwa limetapakaa. Na hapo ndipo tulijua kilichokuwa kimetokea.''

Manusura waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi, inasemekana walikuwa wanawapigia simu majirani na jamaa zao kuwafahamisha hali yao

Aidha Rais Jakaya Kikwete alitembelea eneo la ajali.

Jengo hilo lilikuwa karibu na msikiti pamoja na eneo la makaazi ya watu na nyumba zingine za kibiashara mjini Dar es Salaam.

Polisi wanasema kuwa wanawahoji watu wanne waliohusika na ujenzi wa jengo hilo wakati kukiwa na jengo lengine karibu na lilie liliporomoka ambalo pia walikuwa wanasimamia shughuli za ujenzi wake. Jengo hilo litavunjwa baadaye leo.

Uchumi wa Tanzania unaokuwa kwa kasi umesababisha ujenzi wa kasi mjini Dar es Salaam, katika miaka ya hivi karibuni sawa na ilivyo katika miji mingi ya kiafrika.

Lakini duru zinasema kuwa kasi ya ujenzi na ukosefu wa usalama wakati mwingine inaweka katika hatari maisha ya watu na majengo.