Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), kutangaza kupandisha nauli za daladala, mabasi ya kwenda mikoani, usafiri wa reli na tozo za majini kuanzia Aprili 12, baadhi ya wabunge, wanasiasa, wasomi, wanaharakati na wananchi wa kawaida wamesema hatua hiyo ni ya kuwaongezea wananchi ugumu wa maisha.

Juzi, Sumatra ilisema nauli hizo zimeongezeka kwa kiwango cha asilimia 24.46 na kwamba hatua hiyo imezingatia maoni ya wadau na gharama za uendeshaji.

Wakati Sumatra ikilaumiwa kwa kupandisha nauli hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama hicho kimeunda kikosikazi kwa ajili ya kupitia takwimu ilizotumiwa na wadau kupandisha nauli, baadaye kitatoa msimamo wake, ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali.Kwa upande wake, Mbunge wa Tunduru, Mtutura Mtutura (CCM) alisema muda wa kupandisha nauli haujafika kwa kuwa bei ya mafuta haijapanda.“Hakuna sababu ya kupandisha nauli kwa wakati huu kwa sababu hata gharama za uendeshaji ziko palepale,” alisema Mtutura.

“Wanaomiliki mabasi watueleze kama wameajiri wafanyakazi au wanalazimisha tu mambo,” alisisitiza mbunge huyo.Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema si muda wa mwafaka kwa wamiliki wa mabasi kupandisha nauli na kwamba hatua hiyo, itaathiri nchi kiuchumi.
“Itaongeza gharama za maisha na mfumuko wa bei. Lakini itawaumiza wananchi wa kipato cha chini,” alisema Zitto.


Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba, alisema anafuatilia ili kujua sababu za Sumatra kupandisha nauli na kwamba atatoa taarifa atakapozipata.
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema kupanda kwa nauli kulitarajiwa kutokana na hali halisi ilivyo sasa.
“Ila sina uhakika kama Serikali imejipanga vyema kuwasaidia wananchi maskini,” alisema mtendaji huyo wa NCCR- Mageuzi.
Ruhuza alisema wananchi wa kawaida, watakabiliwa na wakati mgumu na kwamba ili kulimaliza tatizo hilo, Serikali inapaswa kujipanga.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kupanda kwa nauli hizo, kutawaumiza zaidi walalahoi hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa kila kitu kipo juu. Vitu hivyo vinajumuisha kodi ya nyumba, gharama za matumizi ya maji, umeme na vyakula.


“Nchi yetu hivi sasa haina magari ya umma ambayo tungeweza kusema kuwa nauli yake ingekuwa nafuu. Hii inaonyesha kuwa nchi yetu inabaki kuwa na matabaka na walio hoi wataendelea kuwa hoi kwa kuwa hakuna juhudi zinazofanywa ili kuwainua,” alisema Bashiru.Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen-Kijo Bisimba alisema nauli zinapanda wakati wafanyakazi wakiendelea kulipwa mishahara midogo, jambo linalowafanya wazidi kuishi maisha magumu.

“Nadhani Serikali ingepitia upya viwango vya mishahara kwa watumishi wake, ili waweze kumudu gharama za maisha kwa kuwa hivi sasa kila kitu kipo juu,” alisema Bisimba. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema kupanda kwa nauli hizo kunajenga taifa la wananchi wanaokabiliwa na hali ngumu katika kila sekta.


“Mfano nauli za mikoani zimepanda bila huduma kuboreshwa, binafsi nadhani hiyo ilikuwa hoja ya msingi ya Sumatra kukataa kupandisha nauli hizo, Watanzania ni maskini na tunajua wazi kuwa hivi sasa kila kitu bei yake ni juu, leo tena nauli zimepanda, hapa tunatengeneza taifa la walalahoi,” alisema Mtatiro.