Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini imewakamata watu watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na utengenezaji wa vibali bandia vya ukazi kwa wageni wanaishi nchini.
Watu hao walikamatwa hivi karibuni wakiwa na vibali bandia 14 vya ukazi vya daraja B ambavyo kama vingekuwa halali, thamani yake ingekuwa Sh46 milioni.
Watu hao pia walikamatwa na vifaa vinavyotumika katika kughushi vyeti na nyaraka mbalimbali.
Hali kadhalika, mihuri bandia 56 ya taasisi mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Mbaraka Bajenga alisema jitihada za kuwakamata watu hao zilianza baada ya kugundua kuwepo kwa vibali vingi bandia vinavyomilikiwa na raia wa kigeni, bila wao wenyewe kujua.
Alisema Machi 19, mwaka huu, idara ilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye baadaye alisaidia kukamatwa kwa watuhumiwa wengine wawili.

“Watua hawa ni hatari sana, tumewakamata wakiwa na vibali bandia 14 vya ukazi daraja B, stika za bima kwa ajili ya magari, vyeti vya kifo, uzazi na ndoa, stakabadhi za malipo ya Serikali na mihuri 56 na nyaraka nyingine nyingi,” alisema Bajenga
Alisema mihuri bandia iliyokamatwa kuwa ni mmoja wa Idara ya Uhamiaji, saba ya TRA, saba mingine ya Benki ya CRDB, minne ya Benki ya NBC na muhuri mmoja wenye nembo ya Taifa.

Mingine ni muhuri mmoja wa mkurugenzi wa biashara za ndani, mmoja wa msajili msaidizi wa ndoa, mitatu ya Manispaa ya Ilala na mitatu ya Manispaa ya Temeke, minne ya Manispaa ya Kinondoni na mmoja wa Benki ya Exim.

Bajenga aliwataka raia pamoja na wageni wote nchini kufanya uhakiki wa vibali vya ukazi ili kuepukana na adha.  .