Akizungumza kwa hisia kali, Dk Nchimbi alisema si vizuri wanasiasa kueneza chuki kwa kutumia viongozi wa dini kwa sababu kuna siku chuki hizo zitakuwa mbaya kwa taifa.
“Kupitia mkutano huu naomba maaskofu, wachungaji na masheikhe, msikubali kupandikiziwa mbegu za chuki na wanasiasa wanaojitafutia umaarufu kupitia dini,” aliongeza.
Akizungumzia kusambaa kwa maneno ya uchochezi kupitia mitandao ya kijamii alisema: “Ninaomba wazazi tuwaonye watoto wetu na vijana wetu wanaotumia mitandao hiyo vibaya kwani kama itaendelea kuachwa itumike ovyo, itaharibu amani tuliyokuwa nayo kwa zaidi ya miaka 50,” alionya Nchimbi
Katika hatua nyingine, alibainisha kwamba kwa sasa Serikali na vyombo vya usalama vinafuatilia mawasiliano ya simu yanayofanyika hasa yanayolenga kueneza masuala ya udini.
“Nataka niseme kwamba tutachukua hatua kali za kisheria kwa watu wanaotuma na kutengeneza meseji zinazoeneza udini na kujenga chuki kwa Watanzania na sasa tumeanza kuzifuatilia,” aliongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema wamefikia maazimio 16 yaliyotokana na kikao cha majadiliano ya viongozi wa dini huku kubwa likiwa kudumiasha amani ya mkoa huo na taifa kwa jumla.
Maazimio hayo ni kutokuruhusu amani kuchezewa, viongozi wa dini wajihadhari na matamko yanayoweza kuleta mfarakano miongoni mwa jamii na waheshimu imani za wengine.
0 Comments