Mh.Waziri Mkuu Pinda.
*Akemea matumizi mabaya, kupendelea na kujipa tenda
*Ahimiza usimamizi wa fedha wa umma
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amecharuka na kuwakemea watendaji kwenye Serikali za Mitaa
ambao wanatumia nafasi zao kulazimisha kufanya biashara na Halmashauri wanazoziongoza.

Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Mei 9, 2013) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
29 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika hoteli ya Sundown Carnival,
nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Waziri Mkuu alisema haipendezi kusikia baadhi ya wakuu na watendaji katika
Halmashauri wakituhumiwa kuwa sehemu ya mitandao ya wizi katika
Halmashauri au wana maslahi katika kampuni zilizohusika kutoa huduma na bidhaa
duni kwa Halmashauri.

Akitoa
mfano, Waziri Mkuu alisema kuna malalamiko amepokea kwamba Meya wa Halmashauri
moja amefungua kampuni sita na zote anataka zipewe tenda kwenye Halmashauri
anayoiongoza.
“Kuna Halmashauri
zenye taarifa za wizi, upotevu na ubadhirifu ambao kwao umekuwa ni maisha ya
kawaida. ALAT mnayo nafasi kubwa kuendelea kuboresha usimamizi wa fedha za
Halmashauri kwa vile Jumuiya yenu inawaunganisha watendaji wakuu na viongozi
wakuu wa Halmashauri zote chukueni hatua. Waaibisheni na kuwaumbua wale
wanaobanika kutumia vibaya fedha hizi za umma.”
“Lakini, ili
muweze kufanya hayo lazima ninyi wenyewe msiwe sehemu ya uovu huu. Inafadhaisha
sana kusikia minong’ono kuwa baadhi ya madiwani wanatuhumiwa kuwa sehemu ya
mitandao ya wizi katika Halmashauri .... huo ni ukosefu wa wajibu na ni kuvunja
mkataba wenu na umma.

Akuzungumzia
kuhusu utunzaji wa mahesabu, Waziri Mkuu alisema upo udhaifu
katika eneo hilo kwani upo ushahidi unaoonesha kwamba
taarifa za vitabuni hazifanani na kazi iliyofanywa (value for money) akimaanisha kwamba kazi inayofanyika hailingani
na thamani halisi ya fedha iliyotumika.

“Tatizo hili
ni kubwa na lina sura mbili kuu. Moja
ni kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watumishi na madiwani katika usimamizi
wa fedha za Serikali za Mitaa. Baadhi ya madiwani wamediriki  kushirikiana
na watumishi wasio waaminifu katika kuhujumu fedha za umma.  Pili,
ni Watumishi wa Serikali za mitaa kushindwa kutekeleza wajibu wao hivyo kulipwa
mishahara ambayo hawaitumikii ipasavyo,” alisema.

“Hili nalo
nataka lijadiliwe kwa kina na mkitoka hapa kila Kiongozi na Mtendaji ajue ana
jukumu gani la kufanya.  Aidha, hili
ndilo eneo ambalo nataka hatua zichukuliwe ili kunusuru Fedha za Halmashauri,”
alisisitiza.

Alisema kwa
kutambua ukweli huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameendelea
na ukaguzi wa thamani ya fedha zaidi ya ukaguzi wa kawaida.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alipokea hundi ya mfano ya sh. milioni 10 iliyotolewa na Benki
ya NMB ili ziweze kusaidia kununua dawa na vifaa tiba kwa ajili ya majeruhi
wanaoendelea kupatiwa matibabu mkoani Arusha kutokana  na mlipuko wa bomu uliotokea Mei 5, mwaka huu kwenye
Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti.

Akizungumzia
msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Serikali wa benki hiyo, Bibi Domina
Feruzi alisema, kama taasisi wameguswa na maafa yaliyowakumba wakazi hao wa
Arusha na wameamua kuchangia kiasi hicho cha fedha ili kiwasaidie kwa dawa na
vifaa vya tiba vinayohitajika.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, MEI 9, 2013.