Mzee Gurumo akionyesha badhi ya tuzo alizopata katika kazi yake ya Muziki wakati wa mahojiano nyumbani kwake Tabata Makuburi jijini Dar es Salaam. Picha na Kalunde Jamal

 
Dar es Salaam.
 Katika kutambua mchango wa msanii Muhidin Maalim Gurumo kwa jamii na kuuenzi tutakuwa tukiwaletea mfululizo kuhusu nguli huyo, maisha, kazi ya muziki na mikasa kama alivyohojiwa na mwandishi wetu…

“Wakati wa ujana wangu mimi baba yenuuu…shati dukani shilingi sita unapata, kwa hivi sasa shilingi sita hata mkate hupatiii…” Kiitikio kikiwa; “Kwa hiyo wanangu tuishi kutokana na nafasi…”

Hiyo ni sehemu ya mashairi yaliyoimbwa na gwiji la muziki nchini Muhidin Maalim Gurumo zaidi ya miaka 12 iliyopita, akiwa na Bendi ya OTTU Jazz.

Ukweli wa maneno hayo kuhusu ugumu wa maisha unadhihirika hata leo ambapo mamilioni ya Watanzania wana maisha magumu ya kubahatisha kutokana na ufinyu wa kipato.
Hali hiyo inawakumba pia wanaofanya kazi, hata Maalim Gurumo mwenyewe ambaye amefanyakazi akiwa mwanamuziki kwa muda mrefu akisema: “Bado hakuna ninachoweza kujivunia kupitia muziki, hali ya maisha ni ngumu.”

Historia ya maisha Gurumo anayefahamika pia kama Kamanda na mashabiki wa muziki ilianzia mwaka 1940 alipozaliwa, katika Kijiji cha Masaki Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani.

Anaeleza kuwa baada ya kuzaliwa alipata elimu ya msingi, wakati huo pia akisoma madrasa, chuo cha kufundisha elimu ya Dini ya Kiislamu, lakini alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari baada ya baba yake kufariki.

Mjomba chachu ya mafanikio
“Baada ya baba kufariki alinichukua mjomba wangu Selemani Sultani Mikole, wakati huo alikuwa akiishi maeneo ya Ilala Jijini Dar es Salaam,” anasimulia Gurumo.

Anaongeza: “Ukiacha mambo mengine, mjomba wangu huyo ndiye chachu ya mafanikio yangu katika kila jambo, licha ya awali kunizuia nisifanye mambo tofauti, zaidi ya kuijua dini.”

Alipotakiwa kueleza iwapo historia hiyo ya maisha yake inahusiana na wimbo wa Ukiwa alioimba akiwa na Bendi ya Orchestra Safari Sound(OSS) katika mtindo wa Ndekule, Gurumo alisema;

“Ni kweli, wimbo huo una uhusiano moja kwa moja na mjomba wangu na maisha niliyonayo sasa, hata hapa ninapoishi ni yeye alinishawishi ninunue kiwanja hiki. Kwa sasa mjomba wangu ni marehemu, lakini enzi za uhai wake alikuwa akifuatilia mambo yote kuhusu maendeleo ya maisha yangu, namshukuru.”
Yapo maelezo ya watu mbalimbali kuwa enzi za ujana wake kuwa Gurumo aliwahi kufanya kazi ya kuuza maji ya kubeba mabegani iliyotambulika enzi hizo kama ‘Mzega mzega.

Wasimuliaji wanaeleza kuwa alifanya biashara hiyo ikiwa ndiyo kazi yake ya kwanza baada ya kufika jijini Dar es Salaam kwa mjomba wake.

Je, nini ukweli wa maelezo hayo, Gurumo mwenyewe atasemaje? Fuatilia Jumamosi ijayo...

Mwandishi wa makala haya alimuuliza Gurumo: “Nasikia ulivyoingia jijini Dar es Salaam kazi yako ya kwanza ilikuwa kuuza maji kwa mtindo wa mzega mzega?

Kabla ya kujibu swali hilo Maalim Gurumo aliangua kicheko akitingisha kichwa na kujibu: “ Sikuwahi kufanya biashara kama hiyo. Kama nilibeba maji kwa mzega, basi yalikuwa kwa matumizi ya nyumbani kwa mjomba.”
“Hapo ndipo nilipofikia na kuishi kabla ya kuanza maisha ya kujitegemea. Nikiwa kijana wa nyumbani na kwa wakati huo sifa ya kujana ni kusaidia wazazi kutokana na heshima waliyokuwanayo vijana wa wakati huo.”

Gurumo anaongeza: “Kazi ni kazi mradi mkono uende kinywaji, wakati huo hata kama ningepata kibarua cha kulima kwa mraba, ningefanya kwa kuwa nilikuwa kijana na nilikuwa natafuta cha kufanya ili aweze kuendesha maisha yangu.”

Hata hivyo anasema kuwa umaarufu huambatana na mambo mengi ikiwamo watu wengi kujifanya wanakufahamu na kwamba hilo halimpi shida, cha msingi kwake wanaosema hivyo wakiwa ni mashabiki wake anapata faraja.
Anabainisha kuwa kwa enzi hizo hakukuwa na uhaba wa kazi kwani ajira zilikuwa nyingi na asingeweza kukosa kazi ya kufanya, lakini alichagua kuimba kwa kuwa ndiyo alichokiweza.

Kuingia kwenye muziki kwa siri akiwa na umri wa takriban miak 22.

Akizungumzia mwanzo wake kuwa mwanamuziki Maalim Gurumo anaeleza kuwa wazazi wake walikuwa wanamuziki waliopiga muziki wa kiasili wa Kabila la Kizaramo, hasa mama yake aliyepiga ngoma za aina mbalimbali na kuimba, hivyo yeye amerithi kipaji hicho.

Anasema kuwa alianza kujiingiza katika muziki kwa siri na kuimba akiwa chini ya himaya ya mjomba wake marehemu mzee Selemani Sultani Mikole.
Anaeleza kuwa alianza muziki kwa siri kutokana na ugumu wa kumweleza mjomba wake kuwa yeye ameamua kijikita kwenye muziki, akijua kwamba lingepingwa na mjomba wake, hata familia ambayo wakati huo zilikuwa bado hazijawa na mwamko wa masuala ya muziki kwa vijana wao hasa kwa yeye ambaye alikuwa akisoma Madrasa.

Bendi ya kwanza ya muziki wa dansi

Gurumo anasema kuwa bendi yake ya kwanza ilikuwa ni Rufiji Jazz iliyokuwa na maskani yake maeneo ya Fire (Faya) jijini Dar es Salaam.

Anaeleza kuwa ingawa bendi hiyo haikuwa maarufu, lakini hapo ndipo alipojifunzia muziki, akimwongopea mjomba wake kuwa anakwenda madrasa, huku akienda kwenye mazoezi ya muziki wa dansi.

Anasimulia kuwa katika mazoezi hayo alifanikiwa na kuanza kazi ya uimbaji huku pia akiweza kumshawishi mjomba wake kumwacha afanye kazi hiyo.
“Baada ya kujiunga na bendi hiyo ndiyo nilijua mikoa mingi ya Tanzania kwani tulifanya ziara mikoa mingi ikiwamo Dodoma, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Arusha. Wakati huo hapakuwa na upinzani mkubwa, ilikuwa kama amewasili mwanamuziki wa Zaire au kutoka nje,”alisema na kuongeza.

“Mashabiki walikuwa wakijazana kila tunapopiga licha ya kuwa baadhi ya mikoa ilikuwa na bendi zao, huko ndipo nilipozidi kupata ujuzi wa kuimba zaidi na zaidi.”

Itaendelea wiki ijayo